IPA YATAKA MAFUNZO YANAYOTOLEWA CHUONI HAPO YATUMIWE VZR. - Rhevan Media

IPA YATAKA MAFUNZO YANAYOTOLEWA CHUONI HAPO YATUMIWE VZR.

ipa-logo

MKURUGENZI  wa  Chuo Cha Utumishi wa Umma (IPA) Zanzibar , Harusi Ali Masheko amewataka  Wanafunzi  wa Vyuo Vikuu , Watumishi wa Umma na Binafsi kutumia kwa vitendo mafunzo mbali mbali wanayopewa chuoni hapo kama nyenzo ya kuongeza ufanisi wa kiutendaji  katika  utekelezaji wa majukumu yao .
Rai hiyo ameitoa wakati akifunga mafunzo ya Siku mbili ya Itifaki za masuala ya Diplomasia na Maslahi ya Taifa yaliyofanyika  katika chuo hicho kilichopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema kupitia mafunzo hayo washiriki wamepata faida ya kutambua masuala mbali mbali ya Taratibu na miongozo ya Kidiplomasia hasa katika utatuzi wa migogoro mbali mbali inayojitokeza nchini ikiwemo ya ardhi na kisiasa.
Alieleza  faida za mafunzo hayo zitaonekana endapo washiriki watatumia kwa vitendo ujuzi walioupata katika maisha yao ya kila siku na sehemu zao za kazi na vyuoni kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua za kimaendeleo katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kutumia miongozo waliopata kupitia mafunzo hayo kujenga dhana ya uzalendo wa kweli  katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vinavyotokea nchini.
“  Chuo chetu kitaendelea kutoa mafunzo mbali mbali  ya kuwajengea uwezo watendaji mbali mbali wa umma na binafsi pamoja na wanafunzi  kulingana na mahitaji yetu kitaaluma.”, alisema Mkurugenzi huyo.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya maendeleo ya  Vijana ya Chuo hicho(IPAUNC), Mohamed Alian alisema jumuiya hiyo imekuwa ikiratibu mafunzo mbali mbali ya kuinua taaluma za watendaji na wanafunzi wa vyuo vikuu ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa na wataalamu wenye weledi katika masuala ya itifaki na Diplomasia za kimataifa.
Alitoa pongezi kwa chuo na Walimu walioshiriki katika uwasilishaji wa Mada mbali mbali zilizotolewa chuoni hapo, na kuahidi kuwa kutokana na michango, maswali na mijadala iliyotolewa imeonyesha ishara ya ufahamu kwa washiriki hivyo wataweza kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Akizungumza mshiriki wa mafunzo hayo Pandu Salum Sungura, amesema changamoto inayowakabili vijana wengi wa Zanzibar ni ukosefu wa uzalendo hivyo kupitia mada hiyo washiriki hao wataifikisha vizuri taaluma hiyo kwa  jamii.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoratibiwa na Jumuiya ya IPAUNC  yamejumuiya washiriki 120 kutoka taasisi za vyuo vikuu, watumishi wa Umma na Binafsi na zimetolewa mada mbali mbali zikiwemo utatuzi wa migogoro, uzalendo, masuala ya Usalama wa Taifa na Itifaki za Diplomasia za kimataifa.
Previous
Next Post »