HUDUMA YA KWANZ AMAHAKAMANI NI MUHIMU - Rhevan Media

HUDUMA YA KWANZ AMAHAKAMANI NI MUHIMU

MTUHUMIWA AFIA MAHAKAMANI... Wananchi

MTUHUMIWA AFIA MAHAKAMANI... Wananchi wakiangalia gari lillobeba mwili wa mtuhumiwa wa kesi ya dawa za kulevya, Kudra Wincheslaus nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Bukoba, Mkoani Kagera baada ya kuanguka na kufariki dunia wakati shauri lake lilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa jana. Picha na Phinias Bashaya 
Tukio la kufa ghafla mahakamani kwa mwanamke aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kupatikana na madebe mawili ya bangi mjini Bukoba, linapaswa kutufungua macho kuhusu umuhimu wa huduma za afya katika maeneo ya mahakama.
Mkazo mkubwa uko katika hospitali kubwa za rufaa, za mikoa, vituo vya afya na zahanati za vijiji lakini huenda tumesahau kuimarisha huduma ya kwanza.
Katika kipindi hiki ambacho bado huduma za afya hazitoshi kutokana na uhaba mkubwa wa wataalamu yaani madaktari bingwa, madaktari na wauguzi nchi nzima ni vyema, kama jamii, inafaa tukaangalia namna ya kuimarisha na kutumia huduma ya kwanza ambazo katika baadhi ya ofisi zipo kwa jina au boksi lililoandikwa ‘Huduma ya Kwanza’ tu.
Inawezekana katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera huduma ya kwanza ipo kwa boksi lililoandikwa ‘Huduma ya Kwanza’ bila kuwapo huduma maana kama ingekuwapo kiuhalisia, huenda maisha ya mwanamama yule aliyeanguka muda mfupi baada ya kuitwa jalada la kesi yake yasingekuwa hatarini.
Tunasema hivyo kwa sababu, baada ya mshtakiwa huyo mkazi wa Kata ya Kibeta kuanguka, kilichojionyesha wazi ni ukosefu wa utaalamu katika utoaji wa huduma ya kwanza maana baadhi ya wananchi bila shaka wakiwamo maofisa wa mahakama walimsaidia kwa kumpepea, kwa kuwa ni utamaduni uliozoeleka pale linapotokea jambo kama hilo.
Tunaambiwa kwamba waliokuwa wanamsaidia walimwona akipumua kwa nguvu huku wao wakishindwa kujua aina sahihi ya huduma iliyotakiwa kutolewa, hivyo nao wakamshuhudia akipoteza maisha baada ya muda mfupi.
Ndiyo maana tumesema – inawezekana yapo matukio mengine bali hayajulikani kwa vile hayajaandikwa – kwa tukio hili, litufungue macho sote. Kwamba Serikali au taasisi mbalimbali ziweke utaratibu wa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa jamii ili waweze kutoa msaada sahihi na wakati sahihi.
Pia, Serikali na taasisi zihakikishe wanakuwapo wataalamu wa huduma ya kwanza kwenye maeneo muhimu kama Idara ya Mahakama ambako wananchi wengi hufika kwa wakati mmoja.
Tunaamini hili linawezekana kwa sababu Serikali imeweza kusambaza maofisa ustawi wa jamii mahakamani na zaidi katika mashauri yote yanayowahusu watoto kuna watu kwa ajili ya kutoa ushauri.
Tunajua kwamba, kama zilivyo hospitali za rufaa, mikoa, vituo vya afya na zahanati, huduma ya kwanza haizuii kifo lakini husaidia kuokoa uhai, mtu akipatiwa huduma sahihi na haraka.
Kwa kuanzia maofisa hawa ni vyema wakapatiwa mafunzo ya huduma ya kwanza na vifaa ili kuokoa maisha, kupunguza maumivu na kuwapa tumaini wale wanaofikwa na madhara mbalimbali kama vile kuanguka na kuzirai na hata msongo wa mawazo.
Mahakama ya Tanzania ambayo sasa inaendelea na ukarabati na ujenzi wa majengo yake ijaribu kuona uwezekano wa kutenga maeneo maalumu kwa wananchi kukaa wanaposubiri mashauri yao au huduma nyingine za kimahakama kwa kuwa katika baadhi ya majengo yake watu hulazimika kusimama juani au chini ya miti.
Ili kuyaweka maeneo hayo yawe rafiki zaidi wataalamu wa huduma ya kwanza wawepo hapo. Kwa sasa Idara ya Mahakama inaboresha mahakama zake hasa za wilaya na za mwanzo, ambako ndiko kuna matatizo zaidi ya majengo na huduma nyingine za kijamii.

Previous
Next Post »