WANAFUNZI BORA WAFICHUA SIRI YA USHINDI WAO - Rhevan Media

WANAFUNZI BORA WAFICHUA SIRI YA USHINDI WAO

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Feza BoysWanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Feza Boys wakiwa wamembeba mwanafunzi mwenzao Alfred Shauri aliyeshika nafasi ya kwanza katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis 

Dar es Salaam. Kumtumaini Mungu, kujali muda na kuongeza juhudi ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kubeba mafanikio ya wanafunzi waliong’ara katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanywa mwaka 2016.
Matokeo hayo yalitangazwa jana yakibainisha kuwa wavulana na wasichana walifungana katika wanafunzi 10 waliofanya vizuri zaidi, kila jinsi ikiingiza watu watano katika kumi bora.
Wanafunzi waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana walisema kuwa licha ya kusoma katika shule bora, haikuwa rahisi kwao kufaulu kwa kiwango cha juu, kama si kuweka juhudi, kutumia muda vizuri na kujiongeza katika masomo.
Mwanafunzi aliyeshika namba moja kitaifa Alfred Shauri aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari Feza ya Dar es Salaam alisema siri ya mafanikio yake ni kusali, kujali muda na kuweka pembeni kila kitu pale linapokuja suala la masomo.
Akizungumzia matarajio yake alisema familia inamtaka achukue uhandisi, lakini yeye anataka kuwa mfanyabiashara au mwekezaji mkubwa, kwa sababu katika wakati wao hakuna atakayekuwa na wazo la kuajiriwa kutokana na dunia kuwa kijiji, kila mmoja atatafuta namna ya kuajiri wengine.
“Siku zote nimekuwa nikimuomba Mungu nipate mafanikio, naamini na hili ni miongoni mwa mafanikio hayo,” alisema Shauri.
“Licha ya Feza kuwa shule nzuri na ninayoipenda tangu nikiwa mdogo, lakini hilo halikutosha kunifanya nifaulu, zaidi ya kuweka juhudi na kuamini kuwa ninatakiwa niunge mkono juhudi za walimu kwa kusoma kwa bidii ili nifaulu.”
Aliyeshika namba mbili kitaifa Cynthia Mchechu kutoka katika Shule ya Wasichana ya St Francis ya Mbeya alisema amezifanyia kazi ndoto zake na zimekuwa kweli.
Alisema kujali muda, kumuabudu Mungu na kufanyia kazi anachokiamini ndiyo sababu ya mafanikio hayo.
Alisema ndoto inayofanyiwa kazi siku zote huwa na alitamani kufanya vizuri japokuwa hakujua kama ni kwa matokeo hayo, lakini angalau amefikia mafanikio.
Mtoto huyo wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC), Nehemia Mchechu, alifafanua kuwa familia yao ni ya watu wanaofanya kazi katika maeneo ya biashara, hivyo nia yake ni kufuata nyayo hizo.
“Tanzania inakua na itahitaji wanasheria wa majengo na majumba, hivyo nataka kuwa mwanasheria katika nyanja hiyo (legal officer in real estate),” alisema Cynthia.
Pia, mwanafunzi wa shule ya wavulana Marian Boys ya Bagamoyo, Emmanuel Kajege aliyeshika namba 10 kati ya watahiniwa 10 bora alisema kuwa juhudi zake hatimaye zimezaa matunda kama ambavyo amekuwa akiambiwa na wazazi na walimu wake.
Alisema ana furaha kwa sababu angekosa matokeo hayo ingekuwa siku mbaya kwake pengine kuliko siku nyingine kwa kuwa aliazimia kufaulu kwa kiwango cha juu.
“Siyo matokeo niliyotegemea, niliazimia niwe namba tatu bora, lakini kuwa ndani ya 10 bora ni mafanikio kwangu,” alisema Kajege.
Wazazi wafunguka
Akizungumza na gazeti hili mama mzazi wa Alfred Shauri aliyeongoza katika matokeo hayo, Adela Shauri alisema anatambua mwanaye anajituma na alikuwa na matokeo mazuri tangu awali. “Katika mtihani wa darasa la saba alipata alama 227 kati ya 250,” alisema.
Alisema kitu pekee alichojifunza ni kuwahimiza watoto wamtambue Mungu na kwa sababu hiyo imemjenga kijana wake na kumbadili kabisa.
Alisema akiwa darasa la kwanza hadi la tano alikuwa mtundu kiasi cha kumuuliza kama atafaulu, lakini kijana wake alimuahidi atafanya vizuri hadi amshangaze, jambo ambalo lilitokea.
“Alikuwa mtundu tangu mtoto na alipokuwa na umri wa miaka miwili aliwahi kuungua kutokana na utundu, lakini niliamua kumbadili kwa kuhamishia mawazo yake katika misingi ya dini,” alisema.
“Akiwa darasa la tano aliniahidi nisitishwe na utundu wake atafanya vizuri na kweli amefanya vizuri na kunishangaza, lakini shule imemuongezea kujiamini kutokana na kumpa nafasi ya kuonyesha kipaji chake katika mambo mbalimbali.”
Mama mzazi wa Cynthia, Mercy Mchechu alisema kuwa anamshukuru Mungu na amefurahi kwa binti yake kufaulu, lakini furaha yake imepitiliza kutokana na kufanya vizuri kitaifa.
Alisema kama mzazi jukumu lake ni kuhakikisha anamuunga mkono katika kila jambo ili kufikia malengo yake na kutimiza ndoto zake. “Hakuwahi kuniangusha hata siku moja, nashukuru kwa hili, nitamuunga mkono ili afike mbali zaidi,” alisema.
Shule ya kwanza
Mkurugenzi wa shule za Feza, Ibrahim Yunus alisema licha ya wanafunzi kusoma darasani kama ilivyo kwa wengine pia huwapa nafasi ya kushiriki mambo mbalimbali ili kuwaongezea kujiamini.
Alisema Shauri ni miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri pia katika nyanja hiyo ambapo mwaka jana alishinda shindano la insha kwa nchi za Afrika Mashariki. “Lakini vilevile alishiriki mijadala (debates) iliyofanyika Arusha na Croatia,” alisema.

Previous
Next Post »