NEEMA Mfugale, Katibu wa Shirikisho la Vyuo Vikuu la Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma amesema, rushwa ya ngono ni changamoto kubwa inayokwamisha wanafunzi wa kike vyuoni kukubali kuwania nafasi mbalimbali ndani ya CCM,
Mfugale ameyasema hayo jana mbele ya Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT) uliolenga kusikiliza kero za wanafunzi wa kike ambao ni wanachama wa CCM katika vyuo vikuu.
“Wanafunzi wa kike wanashindwa kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama kutokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja rushwa ya ngono na vitisho kila wanapotaka kugombea nafasi hizo,” alisema Neema.
Ameongeza kuwa, “….Lakini pia wanafunzi hawa wa kike wanakabiliwa na changamoto ya kutokujitambua, uoga na tabia ya kutopendana jambo ambalo linawakatisha tamaa ya kugombea nafasi mbalimbali.”
Neema amedai kuwa bado wanafunzi wa kike hawana ujasiri wa kukabiliana na fitna pamoja na hujuma katika michakato ya uchaguzi, ndiyo maana wamekuwa wakisuasua kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali.
Akijibu hoja hizo, Dk. Tulia alisema suala la rushwa ya ngono lipo na linafahamika lakini inategemea na utashi binafsi wa msichana pamoja na msimamo alionao.
Dk. Tulia amesema, “Ili wanafunzi wa kike na wanawake kwa ujumla waweze kuepukana na tatizo la rushwa ya ngono katika chaguzi za ndani ya CCM ni lazima wawe na misimamo pamoja na kujiamini katika kile wanachokifanya.
“Jinsi mdada alivyojiweka ndiyo inaweza kumfanya kuwa mhanga wa rushwa ya ngono. Kwa mfano kama mtu hatakuwa na bidii ya kusoma kamwe hawezi kujiamini wala kuwa na uhakika na uwezo wake na hivyo ni rahisi kujiingiza katika rushwa ya ngono.”
Dk. Tulia amewaasa wanafunzi wa kike akisema, “Ukikubali kutoa rushwa ya ngono kwa kiongozi wa chama ili upate nafasi ya uongozi utafanya hivyo kwa watu wangapi na utakuwa binti wa aina gani? Ni vyema kujiamini na kuwa makini.”
Sign up here with your email