WATUMISHI wastaafu wa serikali wanaolipwa na serikali kupitia wizara ya fedha na mipango wameitaka serikali kurekebisha viwango vya malipo ya pensheni wanayolipwa sasa kufuatia kupanda kwa gharama za maisha ambako hakuendani na hali halisi ya malipo wanayolipwa.
Wakizungumza katika zoezi la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa na wizara ya fedha na Mipango linaloendelea mkoani Kigoma, Wastaafu hao wamesema kuwa kwa sasa kiwango wanacholipwa wastaafu waliostaafu utumishi wao muda mrefu hakiendani na malipo yanayotolewa kwa wastaafu waliostaafu hivi karibuni.
Shaban Funenge mstaafu wa jeshi la wananchi wa Tanzania alisema kuwa wastaafu wengi ambao wamestaafu kwa zaidi ya miaka 10 wamekuwa na manung’uniko sana na kwamba serikali haina budi kufanya maboresho kwa wastaafu hao na kuondoa tofauti zao.Akizungumzia zoezi la Uhakiki linaloendelea Patrick Maganga alisema kuwa zoezi limekuja wakati muafaka ambao malalamiko ya wastaafu yamekuwa mengi na kwamba ametaka zoezi hilo liende sambamba na maboresho ya malipo kwa wastaafu hao.
Kwa Upande wake Emilia Maibori ambaye ni Mwalimu Mstaafu alisema kuwa mafao ya wastaafu yanapaswa kutolewa kwa wakati muafaka badala ya wastaafu kulalamika kufuatia kucheleweshwa kwa malipo hayo akieleza kuanza kupata malipo hayo mwaka 2015 kuafuatia kushindwa kupata malipo hayo tangu mwaka 2005 alipostaafu ambapo ameeleza kuridhishwa na zoezi la uhakiki linaloendelea.
Akieleza kufanyika kwa uhakiki huo Mkaguzi Mkuu Msaidizi wa ndani wa serikali,Stanslaus Mpembe alisema kuwa kwa zaidi ya mikoa 21 ambayo uhakiki huo umefanyika mafanikio yamekuwa makubwa na idadi kubwa ya wstaafu wamekuwa wakijitokeza.Mpembe alisema kuwa licha ya wastaafu wanaojitokeza pia serikali imetoa fursa kwa wastaafu ambao wamelazwa kwenye hospitali mbalimbali kufikiwa na watumishi wanaoendesha zoezi hilo na kwamba ndugu wa wastaafu hao wametakiwa kujitokeza kutoa taarifa za wastaafu hao ili waweze kufuatwa maeneo walikolazwa.
Wakati zoezi likiendelea mikoa mbalimbali nchini Mkaguzi huyo alisema kuwa baada ya zoezi kupita kwenye mkoa husika wastaafu ambao hawajahakikiwa wanatakiwa kujiorodhesha kwenye ofisi za hazina ndogo za mikoa waliyopo kabla ya muda wa zoezi hilo haujamalizika.
Naye ofisa habari wa Wizara ya Fedha na Mipango Ben Mwaipaja amewataka watumishi waastafu kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la uhakiki kwenye mikoa yote watakayo pita.
"Mpaka sasa tumeshapita jumla ya Mikoa 21 bado mikoa ya lindi,Mtwara na Zanzibar ambapo napo zoezi litaendelea ninawaomba wastaafu wajitokeze ili wasije poteza haki zao"alisema Mwaipaja.
WATUMISHI wastaafu wa serikali wanaolipwa na serikali kupitia wizara ya fedha wakifanyiwa uhakiki mkoani Kigoma. WATUMISHI wastaafu wa serikali wanaolipwa na serikali kupitia wizara ya fedha wakifanyiwa uhakiki mkoani Kigoma
Sign up here with your email