ZANZIBAR KUAGIZA MCHANGA NJE YA NJE - Rhevan Media

ZANZIBAR KUAGIZA MCHANGA NJE YA NJE


Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema inakusudia kuagiza mchanga kutoka nje ya visiwa hivyo kwa matumizi ya ujenzi kutokana na rasilimali hiyo kupungua kwa kasi.
Waziri Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohamed alisema hayo jana alipotoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kuwapo kwa uhaba wa mchanga Zanzibar. Alisema Serikali imeshaanza mazungumzo na baadhi ya nchi kuhusu upatikanaji wa rasilimali hiyo ambayo itasaidia kuondokana na uchimbaji mchanga holela unaoweza kusababisha maafa.
Hamad alisema utafiti wa Serikali umegundua kuwapo uharibifu wa mazingira katika maeneo yote ya Unguja na Pemba yanayochimbwa mchanga, ikiwamo maji kupanda juu, kuharibika kwa vyanzo vya vyake, kuwapo mashimo na ukosefu wa maeneo ya kilimo kwa wananchi.
Alisema takwimu za Idara ya Misitu na Maliasili zinaonyesha katika miaka 10 kuanzia 2005 – 2015, maeneo ya Unguja yalichimbwa tani 2,658,503 na Pemba tani 200,959 za mchanga kutoka machimbo rasmi yaliyoidhinishwa na Serikali.
Waziri Mohamed alisema kiwango hicho ni sawa na wastani wa tani 241,682 kwa mwaka kwa Unguja na tani 18,269 kwa Pemba, ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na hali ya ukubwa wa Zanzibar.
Alisema pia ni kikubwa ikilinganishwa na eneo la hekta 14, lililobaki ambalo ni dogo na halitoshi kwa matumizi ya uchimbaji wa mchanga kwa ajili ya ujenzi. Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali ya Zanzibar imeamua kuchukua hatua za udhibiti wa uchimbaji mchanga uliobaki ili kuinusuru nchi kuwa sehemu hatarishi.
Alisema miongoni mwa hatua hizo ni kuandaa mpango wa kuagizia mchanga kutoka nje ya Zanzibar, kuelimisha kuhusu utaalamu wa matumizi ya rasilimali mbadala ya mchanga, kuandaa mikakati ya utoaji vibali vya uuzaji na uchimbaji mchanga kwa wenye magari na masuala mengine ambayo wanaamini kwamba yatasaidia kukabiliana na hali hiyo.
Hamad alisema tayari wameshakutana na wadau wanaohusika na masuala ya rasilimali ya mchanga, wakiwamo wataalamu, wamiliki wa magari ya mchanga, wamiliki wa miradi ya nyumba na Serikali ili kulifanyia kazi suala hilo haraka iwezekanavyo.
Uamuzi huo umepokewa kwa hisia tofauti na wadau, akiwamo Msabaha Hassan Silima, ambaye ni mwenyekiti wa wenye magari ya kubeba mawe na mchanga Zanzibar, aliyeomba muda zaidi wa kujipanga ili kutafuta mbadala wa shughuli hizo.
Alisema kazi hiyo huwaingizia mapato katika maisha yao, hivyo ni vyema mabadiliko yoyote yanayotarajiwa kufanywa na Serikali yakangalia na masilahi yao.
Hata hivyo, alisema wanaunga mkono uamuzi huo kutokana na uharibifu unaotokana na uchimbaji mchanga na mawe kuathari watu wote.
Mmoja wa wamiliki wa magari hayo, Makame Juma alisema pamoja na Serikali kutangaza nia ya kuagiza mchanga kutoka nje ya Zanzibar, bado wanahitaji kupewa nafasi ya kuendesha biashara hiyo.
Alisema itakuwa ni jambo la kushangaza kwa Serikali kutoa agizo kwa wamiliki wa magari ya mchanga kuachana na kazi hiyo bila kutafutiwa shughuli mbadala ya kuendesha maisha yao. Aliiomba Serikali kukaa na wadau wa masuala ya ardhi na wamiliki wa magari kuhakikisha suala hilo linafanyika katika hali ya amani kwa pande zote mbili.

Previous
Next Post »