Mtaalamu wa lishe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Mariam Nyamwaira akizungumza na waandishi wahabari leo.
…………………………………………………………..
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inaadhimisha wiki ya lishe kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuzingatia lishe bora ikiwamo kupima wingi wa mafuta mwilini.
Maadhimisho hayo yana lenga kupunguza magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, magonjwa ya figo na saratani.
Mtaalam wa lishe kutoka katika hospitali hiyo, Mariam Nyamwaira amesema katika maadhimisho hayo, wataalamu wa lishe watapata fursa ya kutoa ushauri kuhusu suala la lishe, uhusiano wa lishe na mazoezi, kupima urefu na uzito pamoja na kupima wingi wa mafuta mwilini .
“Lengo ni kuweka uelewa wa suala la lishe kwani ulaji usiofaa unachangia kwa kiasi kikubwa watu kupata magonjwa yasiyoambukiza hivyo kupitia wiki hii tunatoa huduma bure na endapo mtu akibainika kwamba katika hali hatarishi tutamuingiza kwenye kliniki zetu ambazo zinafanyika hapahapa Muhimbili ,”amesema Bi Nyamwaira.
Leo jumla ya watu 78 wamepimwa wingi wa mafuta mwilini na kupewa ushauri wa lishe bora na kati ya hao asilimia 85 wapo hatarini kupata magonjwa yasioambukiza kutokana na kuzidi uzito.
Maadhimisho hayo yameanza Januari 30, 2017 na yatahitimishwa Februari 03, 2017.
Sign up here with your email
