Mwili
wa ofisa mtendaji wa mtaa wa Kabwe, katika kata ya Iyela jijini Mbeya
Clementine Enock (34) umekutwa ukiwa umetelekezwa katika eneo la Airport
ya zamani baada ya kuuawa na watu wasiofahamika kwa kubanwa pumzi.
Kamanda
wa polisi mkoani Mbeya Dhahiri Kidavashari alisema jana kuwa walibaini
kuwepo kwa mwili huo Januari mbili, mwaka huu majira ya saa moja asubuhi
baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Kidavashari
alifafanua kuwa kabla ya tukio hilo marehemu aliondoka nyumbani kwao
siku ya Mwaka mpya na kuaga kuwa anakwenda Airport kwenye sherehe ya
rafiki yake huku akiwa na gari yenye namba za usajili T234 DJM aina ya
Toyota Spacio.
Alisema
kuwa ndugu wa marehemu walipata hofu mara baada ya ndugu yao kuchelewa
kurudi nyumbani na ndipo wakaanza kumpigia simu bila mafanikio mpaka
usiku wa manane.
“Marehemu
aliaga nyumbani kwao Uyole ya Kati alikokuwa akiishi majira ya saa kumi
jioni siku ya tarehe moja kwa madai anaenda kwenye sherehe ya rafiki
yake akiwa na usafiri wa gari lake, ambapo mpaka kufika usiku wa manane
hakukuwa na taarifa yeyote ndipo hofu ikatanda kwa familia ambapo
walipiga simu kwa ndugu jamaa na marafiki na kueleza kuwa hawajui
alipo,” alisema Kidavashari.
Kwa
mujibu wa Kamanda Kidavashari siku iliyofuata majira ya saa moja
asubuhi mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umetupwa katika eneo la wazi
jirani na Shule ya Sekondari ya Samora ambapo uchunguzi wa awali
unaonesha kifo chake kilitokana na kubanwa pumzi na watu wasiofahamika.
Alisema
mazingira ya kifo yanaonyesha wazi kuwa marehemu aliuawa na mtu wa
karibu yake huku akisema tukio hilo lilifanywa ndani ya nyumba ya mtu.
Sign up here with your email