WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, ameziagiza taasisi zote za Serikali kuhakikisha zinahifadhi taarifa zao katika Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu (IDC) kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam.
Profesa Mbarawa amezitahadharisha taasisi zenye mpango wa kujenga na kuanzisha vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu kuacha mara moja mpango huo, kwani kufanya hivyo ni kuingilia kazi ya kituo hicho na kupoteza fedha za Serikali.
Waziri Mbarawa alisema hayo mara baAda ya kutembelea kituoni hapo na kupokea taarifa ya uendeshaji kutoka kwa mkuu wa kituo, Abdul Mombokaleo.
“Sioni sababu kwa taasisi nyingine kutaka kujenga vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu, Serikali imeshawekeza fedha nyingi kwa ujenzi wa kituo hiki, hivyo taasisi zote nchini zinalazimika kutumia kituo hiki,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisisitiza kampuni zilizo chini ya wizara yake kuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine kwa kuwa wa kwanza kupeleka taarifa zao kuhifadhiwa katika kituo hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo hicho, Mombokaleo, alisema kuwa hadi sasa wameshafanikiwa kuunganisha wateja 13 katika kituo hicho na wengine zaidi ya 40 wapo kwenye mchakato wa kujiunga.
Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa alitembelea ofisi za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kusema kuwa ameridhishwa na utendaji wake kutokana na jitihada zake za kuteka soko la ushindani miongoni mwa kampuni za mawasiliano nchini.
Sign up here with your email