Elimu ni nguzo imara ya mafanikio kwa mtu binafsi na hata kwa maendeleo ya taifa lolote.
Wakati Tanzania inapata uhuru, Rais wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere alisema kuna maadui wakubwa watatu wa maendeleo ambao tunapaswa kupambana nao. Aliwataja kuwa ni ujinga, maradhi na umasikini.
Kimsingi, adui ujinga anawabeba wenzake waliobaki. Hapa namaanisha mtu akifanikiwa kuondokana na ujinga, ni rahisi kwake kupambana na maradhi na umasikini.
Njia rahisi ya kuondokana na ujinga ni kupitia elimu inayotolewa ama katika taasisi za elimu au katika mazingira mengine yasiyo rasmi.
Hata hivyo, kwa muktadha wa makala haya, nazungumzia elimu ya mfumo rasmi inayomlazimisha msomaji kukutana na mwalimu kwa minajili ya kumtoa ujinga.
Pamoja na umuhimu wao, walimu hasa wale wanaopangiwa kazi katika maeneo ya pembezoni, wanakabiliwa na changamoto nyingi.
Matokeo yake kila anayepangiwa huko anatamani aombe uhamisho hasa wa kwenda mijini na maeneo mengine yenye ahueni.
Uhamaji wa walimu katika maeneo ya vijijini umesababisha shule za vijijini kujikuta zikibakiwa na walimu wachache, hivyo kuathiri maendeleo ya elimu kwa kiwango kikubwa.
Hali ni tofauti mijini kwani walimu wanalundikana na haishangazi kuona mwalimu akilazimika kufundisha vipindi vichache, ilhali vijijini walimu wameelemewa na mzigo.
Mwaka jana nilibahatika kufanya ziara katika wilaya za Morogoro Vijijini na Mvomero, mkoani Morogoro. Hali niliyokutana nayo inasikitisha.
Katika kijiji cha Kibuko kilichopo wilayani Morogoro Vijijini, uongozi ulinieleza kuwa katika shule nne zilizopo walimu wake hawazidi 20. Hizo ni shule zenye wanafunzi kuanzia 400 hadi 800. Kilichopo ni kuwa walimu wanaopangiwa kazi hapo, hawadumu kwani huhama.
Katika Wilaya ya Mvomero, hali pia haikuwa shwari kwani katika shule moja yenye wanafunzi 800, walimu walikuwa watatu pekee!
Wakati haya yanatokea vijijini, maofisa elimu, viongozi wa Serikali na hata wanasiasa wamejazana mijini.
Inawezekana wameridhika na hali iliyopo, ndiyo maana hawaoni haja ya kuzifanyia kazi changamoto hizi zinazowakabili walimu wetu.
Hii ni changamoto kubwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imedhamiria kufufua elimu kwa kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya elimu.
Hata hivyo, juhudi hizi zilizochagizwa na mpango wa elimu bure ambao sasa tunaona ukihanikiza pia utengenezaji wa madawati, hazitokuwa na tija kama walimu hawatokuwapo shuleni.
Kwa mtazamo wangu, kabla ya kugeukia miundombinu kama ujenzi wa madawati, Serikali ingewekeza vilivyo kwa walimu ambao kimsingi ndio roho ya elimu shuleni. Ihakikishe shule zote hasa zile za pembezoni zina walimu kwa idadi sawa na wenzao wa mijini.
Ili kuhamasisha walimu kukubali kufanya kazi katika maeneo haya, naiomba Serikali itekeleze kwa vitendo ahadi yake ya kutoa motisha ya kifedha kwa walimu wanaofundisha katika maeneo yenye mazingira magumu.
Ikumbukwe kuwa ahadi hii ilitolewa bungeni wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Kwa kuwa Serikali ya sasa inajinasibu na kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu, nadhani huu ni wakati mwafaka wa kutekeleza ahadi hii kwa ajili ya kuokoa hali ya mambo katika shule za pembezoni.
Naamini hata kiasi kidogo kikitolewa kwa walimu, kinaweza kuwapa ari ya kuishi vijijini.
Amina Juma ni mwandishi wa Mwananchi Morogoro
Sign up here with your email