MWAKYEMBE KUWASILISHA MUSWADA WA KIHISTORIA BUNGENI - Rhevan Media

MWAKYEMBE KUWASILISHA MUSWADA WA KIHISTORIA BUNGENI

Dk.-Harrison-Mwakyembe


Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe atawasilisha Bungeni wiki ijayo muswada wa kihistoria wa msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za mawakili katika kutetea na kupigania haki zao nje na ndani ya mahakama.
Jumatano wiki hii Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilimaliza zoezi lililochukua wiki nzima la kukutana na wadau mbalimbali wa sheria kubadilishana nao mawazo kuhusu muswada huo na baadaye kumwita Dk. Mwakyembe kujibu baadhi ya changamoto zilizojitokeza.
Katika kuhitimisha zoezi hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, alimpongeza waziri huyo kwa kuzingatia kwa karibu maoni ya wadau na Kamati, hatua ambayo itawezesha muswada huo kupita bila upinzani mkubwa.
Sheria ya Msaada wa Kisheria itawezesha kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania wananchi wasio na uwezo wa kuhudumiwa na mawakili kwenye masuala ya kisheria kupata msaada huo kutoka kwenye vikundi mbalimbali vya msaada wa kisheria vitakavyokuwa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima.
Maelfu ya vijana waliomaliza sekondari na vyuo mbalimbali watapatiwa mafunzo maalum ya kisheria na kutambuliwa rasmi kuwa wasaidizi wa kisheria watakaosambazwa mijini na vijijini kutoa huduma hiyo.
Mitaala ya mafunzo hayo iliishaandaliwa na Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) na hadi sasa zaidi ya vijana 4,700 wameshapitia mafunzo hayo.
Akihojiwa mjini Dodoma jana, Dk. Mwakyembe alisema sheria hiyo itakuwa mkombozi kwa wanawake wengi nchini wanaonyanyaswa na taratibu za kimila zilizopitwa na wakati kwenye masuala ya ndoa, talaka, mirathi, umiliki wa ardhi, uasilia wa watoto na kadhalika.
“Itakuwa mkombozi kwa wanyonge wote wakiwemo watoto yatima, wazee, wajane, walemavu na kadhalika, wanaodhulumiwa kwa kutokujua sheria na haki zao”.
Previous
Next Post »