MUSWADA WA SHERIA MPYA YA MADAKTARI WAZUA HOFU - Rhevan Media

MUSWADA WA SHERIA MPYA YA MADAKTARI WAZUA HOFU

Picha inayohusiana



 MADAKTARI wasaidizi na matabibu wameishauri Serikali kutafakari uamuzi wake wa kutowatambua kama madaktari katika Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Watalaamu wa Afya wa Mwaka 2016, kwa kuwa utasababisha vifo na kuathiri watu wengi kwa kukosa huduma ya afya.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya madaktari hao walisema hadi sasa idadi ya madaktari wasaidizi nchini (AMO) ni 3,040 wakati wale madaktari wenye shahada (MD) wakiwa hawafikii hata nusu yao, hivyo wao wamekuwa wakihudumia sehemu kubwa ya wagonjwa.
Akielezea uamuzi wa Serikali juzi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema kuwa licha ya kuthamini mchango wao wa kutoa huduma za afya nchini, wizara yake imekataa mapendekezo yao ya kuitwa madaktari kwa kuwa sifa muhimu ya kuitwa daktari ni shahada ya kwanza ya udaktari inayotambulika.
Akizungumzia muswada huo, Dk. Donald Musumu, alisema uamuzi wa Ummy katika muswada huo umeonyesha kukataliwa kwa mapendekezo 18 kati ya 37 yaliyowasilishwa na wadau, wakitaka madaktari wasaidizi kuendelea kutambuliwa, hivyo watakoma kuwa madaktari na kutoa huduma.
“Waziri ametamka kuwa katika mapendekezo aliyowasilisha lile la kuwatambua madaktari wasaidizi limekataliwa, hivyo tafsiri yake ni kuwa iwapo muswada huo utapitishwa, basi utawaathiri madaktari wasaidizi wengi ambao watakoma kutoa huduma na kufunga hospitali zilizofunguliwa kwa vyeti vyao.
“Kwa mujibu wa muswada huo, madaktari wasaidizi watakoma kuendelea kutoa huduma na watakaobainika wakitoa huduma na kufanya upasuaji watashtakiwa na kutozwa faini ya shilingi milioni tano, jambo hili Serikali inapaswa kuangalia kwa makini kwa kuwa wamekuwa wakitegemewa kwa huduma za upasuaji wa dharura kwa wajawazito vijijini ambako hakuna madaktari wenye shahada,” alisema Dk. Musimu.
Alisema ni mapema mmno kupitisha sheria inayowaengua AMO kuendelea kutoa huduma na kubaki na MD pekee ambao bado hawatoshelezi mahitaji ya utoaji huduma na kubainisha jambo hilo litaathiri huduma ya afya kwa ujumla.
“Muswada huo unatuita wahudumu shirikishi na kunyang’anywa leseni zetu, hivyo hatutaweza kutibu, ni kwanini Serikali isifikirie upya jambo hili? Kama tulionao hawatoshi kutoa huduma kwa nchi nzima unawapotezaje na hawa kidogo ulionao ambao wamekuwa wakisaidia kuokoa maisha ya Watanzania?” alisema na kuhoji.
 WAJIANDAA KUKUTANA
Akizungumza jana kwa simu, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Wasaidizi, Madaktari Wasaidizi wa Meno, Matabibu na Matabibu Wasaidizi, (AMEPTA), Dk. Francis Ngonyani, alisema taarifa iliyotolewa na Ummy imewastua madaktari hao na kwamba wanajiandaa kukutana ili kutoa tamko lao.
Previous
Next Post »