MAWAZIRI WACHEKELEA MIKATABA TISA WALIYOISAINI NA UTURUKI - Rhevan Media

MAWAZIRI WACHEKELEA MIKATABA TISA WALIYOISAINI NA UTURUKI


BAADHI ya mawaziri wameielezea mikataba tisa ambayo Tanzania imeingia makubaliano na kusaini na nchi ya Uturuki na kubainisha kuwa, mikataba hiyo, imelenga kuongeza zaidi ufanisi wa kiutendaji katika sekta za afya, elimu, kilimo, uchukuzi, diplomasia, utalii , viwanda na ulinzi.

Mawaziri hao waliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu undani wa mikataba waliyoisaini juzi wakati wa ziara ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan iliyomalizika juzi jioni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema katika mkataba aliousaini utawezesha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha dawa.

Aidha, alisema kupitia mkataba huo, pia nchi hiyo ya Uturuki itawezesha mafunzo ikiwemo kubadilishana uzoefu kwa madaktari bingwa wa magonjwa sugu kama vile figo, saratani na moyo, hali itakayoongeza idadi ya madaktari bingwa nchini waliobobea katika kutibu magonjwa hayo.

“Lakini pia watatusaidia kupata mafunzo ya kutumia katika hospitali zetu mfumo wa udhibiti wa taarifa za hospitali (HMIS) ambao ni wa kieletroniki unaotumika kuhifadhi taarifa zote za wagonjwa na takwimu za wagonjwa wa magonjwa mbalimbali,” alifafanua Ummy.

Alisema kupitia mfumo huo, kwa sasa itakuwa ni rahisi Serikali kupata takwimu ya magonjwa mbalimbali kama vile kifua kikuu na moyo lakini pia mfumo huo utarahisisha katika eneo la ukusanyaji mapato kwa kuwa mfumo mzima uko wazi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema mkataba aliousaini umelenga katika kuikuza sekta ya utalii nchini ambapo nchi hizo mbili zote kwa pamoja zitakuwa na ushirikiano katika kutangaza utalii unahusu pande zote mbili.

“Lakini pia tutabadilishana wataalamu kwa lengo la kujifunza na kuongeza ujuzi katika eneo la sekta ya utalii, tutaangalia namna wenzetu walivyofanya hadi kufanikiwa kuvutiwa idadi kubwa ya watalii kuliko sisi ambao tuna vivutio vingi vya utalii lakini tunapokea watalii wachache,” alifafanua.

Alisema kwa takwimu zilizopo Uturuki inapokea watalii takribani milioni 10 kwa mwaka wakati Tanzania inapokea kwa sasa watalii milioni moja kwa mwaka pekee.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alisema amesaini mkataba wa ushirikiano baina ya Tanzania na Uturuki katika eneo la kubadilishana uzoefu kwenye kilimo.

Alisema Uturuki ni nchi ya saba duniani katika kuzalisha mazao ya kilimo na kwa kuwa Tanzania takribani asilimia 80 ya wakazi wake wanajishughulisha na kilimo, hiyo ni fursa nzuri ya kuikuza sekta hiyo kwa manufaa ya taifa na wananchi kwa ujumla.

Aidha, alisema kwa upande wa teknolojia, nchi hiyo ni moja ya kati ya nchi zinazoongoza duniani katika masuala ya teknolojia hivyo kupitia mkataba huo, Tanzania itanufaika kwa kupata mafunzo mbalimbali katika eneo hilo la teknolojia.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kupitia mkataba aliousaini wamekubaliana kushirikiana na nchi hiyo katika eneo la kuendeleza viwanda ambapo nchi hiyo itaanzisha viwanda mbalimbali hapa nchini kikiwemo kiwanda cha nguo.

Aidha alisema kupitia mkataba wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda vidogo (SIDO) na shirika la viwanda vya Kati Uturuki, mkataba huo unahusu makubaliano ya kupatiwa mafunzo, ikiwa ni pamoja na kubadilishana wataalamu kwa lengo la kuongeza ujuzi na uzoefu.

Mikataba iliyosainiwa ni pamoja na mkataba wa ushirikiano baina ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na shirika la ndege Uturuki, ushirikiano baina ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji Uturuki na mkataba wa ushirikiano katika maendeleo baina ya nchi hizo mbili.

Mikataba mingine ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya elimu na utafiti, ushirikiano baina ya Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) na Shirika la Viwanda vya Kati Uturuki na ushirikiano katika sekta ya Utalii kwa nchi zote mbili.
Previous
Next Post »