KATIBU TAWALA WA MKOA WA MOROGORO,AWAASA WAKURUGENZI KUTUMIA VYEMA FEDHA ZA MIFUMO - Rhevan Media

KATIBU TAWALA WA MKOA WA MOROGORO,AWAASA WAKURUGENZI KUTUMIA VYEMA FEDHA ZA MIFUMO

UYUOKatibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt.John Ndunguru akiongea na wakurugenzi wa Halmashauri wa mikoa minne walioshiriki Warsha Mkoani hapo.UYUOOO
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt.John Ndunguru wa nne kutoka kulia walio kaa na wa pili kutoka kushoto ni DKT.Charles Mhina akiwa na wakurugenzi wa Halmashauri katika picha ya pamoja.
…………….
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. John Ndunguru, amewaasa  Wakurugenzi wa Halmashauri wa Mikoa Minne wanaoshiriki Warsha Mkoani hapa, kutumia vema fedha wanazopelekewa ambazo ziko chini ya Mfuko wa LDGD ili Serikali iweze kufikia lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt.  Ndunguru ameyasema hayo mwanzoni mwa wiki hii wakati akifungua Warsha ya siku tatu ya utambulisho wa Miongozo Mikuu ya Mfumo utakaotumika katika Kuzipatia  Ruzuku ya maendeleo Mamlaka za Serikali za Mitaa hapa nchini.
Amesema, Wakurugenzi wanapashwa kusimami miongozo hiyo iliyotolewa na ambayo wataelekezwa wakati wa warsha hiyo ili kuhakikisha kuwa malengo ya uanzishwaji wa Mfumo huo yanatekelezwa ambayo ni kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, Dkt. Ndunguru amewataka Wakurugenzi hao  kuacha mazoea ya kubaki na fedha nyingi za Mfuko wa LDGD bila kuzitumia kwa wakati, jambo alilosema linawacheleweshea wananchi maendeleo wanayoyahitaji.
“Usifikiri kuziweka hela  kwamba ni utendaji kazi mzuri…na wewe ni jipu. ukitumia fedha hizo vibaya ni jipu, lakini pia ukiziacha bila kuzitumia ni jipu jingine tena jipu baya zaidi kwani unawakosesha wananchi huduma” alisisitiza  Dkt. Ndunguru.
Nae Mshauri Mkuu kwa niaba ya Shirika la Maendeleo la Japan hapa nchini (JICA)    Bw. Michiyuki Shimoda, amewataka washiriki wa Warsha hiyo kujifunza kwa umakini  miongozo inayohusu “Local Gornvement Development Grant” ambayo itapitiwa katika kikao hicho. Amesema wanatakiwa kuwa makini katika kujifunza miongozo hiyo kwa kuwa wao ndio watumiaji wakubwa  nia ikiwa ni kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Serikali za Mitaa Utawala Bora OR – TAMISEMI Dkt. Charles Mhina, amesema lengo la warsha hiyo ni kutoa Elimu ya namna ya kufanya ufuatiliaji wa shughuli zote ambazo zinafadhiliwa chini ya Mfuko wa LDGD.
Warsha hiyo ya Siku tatu inafanyika katika Ukumbi wa Edem katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na inashirikisha Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Mipango na Uchumi, baadhi ya Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti za Mikoa, Waweka Hazina na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Mikoa minne ya Dodoma, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Previous
Next Post »