Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema anakaribia kukamilisha kuandaa mpango ambao utachukua nafasi ya mpango wa bima ya afya wa Obamacare.
Akiongea wakati wa mahojiano na gazeti la Washington Post, Bw Trump, ambaye ataapishwa kuwa rais wa Marekani Ijumaa wiki hii, amesema mpango wake utajumuisha kila mtu lakini gharama yake itakuwa ya chini.
Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi.
Amesema anatarajia kuidhinishwa kwa Bw Tom Price, ambaye amependekeza awe waziri wake wa afya, kabla ya kuzindua rasmi mpango huo wake.
Bw Trump pia amedokeza kwamba kampuni za kutengeneza dawa zitalazimishwa kushauriana moja kwa moja na serikali kuhusu bei za dawa za kutumiwa chini ya mpango wa afya wa Medicare na Medicaid.
Ijumaa wiki iliyopita, Bunge la Wawakilishi liliidhinisha hatua ya kwanza katika kuubadilisha mpango huo wa Obamacare siku moja baada ya Seneti kuidhinisha hatua sawa.
Hivi majuzi, Rais Obama aliwahimiza wanachama wa chama cha Democratic kupigania sheria hiyo ambayo utawala wa Donald Trump umeahidi utaibatilisha upesi baada ya kuingia madarakani.
Kwenye mkutano wa faraghani wa saa mbili, Bw Obama aliwahimiza wabunge wa chama hicho kuitetea sheria hiyo, huku wanachama wa Republican nao wakichukua hatua kufuta sheria hiyo.
Sheria hiyo iliwezesha takriban Wamarekani 20 milioni zaidi kupokea huduma ya afya.
Hata hivyo, sheria hiyo imekabiliwa na changamoto za kupanda kwa malipo ya wanaopokea huduma ya bima na pia kampuni nyingi za bima zimejitoa kutoka kwa mpango huo.
Hilo limewaacha Wamarekani wakiwa hawana njia nyingi mbadala za kujipatia bima ya afya.
Sign up here with your email