Chuo Kikuu cha Bagamoyo ( UB) , kimesema kipo mbioni kuanzisha Taasisi ya Maadili chuoni hapo ambayo itakuwa na kozi ya Maadili na kila mwanafunzi bila kujali fani atalazimika kuisoma kozi hiyo .
Hayo yamesemwa mapema leo 28 Januari 2017 na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Costa Mahalu wakati wa sherehe ya kukabidhi wanafunzi washindi wa shindano la kuandika Insha liloandaliwa na Taasisi ya kiraia toka nchini Kenya ya Fahamu kwa ushirikiano na UB.
Tukio hilo limefanyika makao makuu ya chuo hicho Kawe Beach Dar Es Salaam huku pia ikiuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la chuo, Jajyi Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Dk. Stephen Bwana.
Katika tukio hilo, Profesa Mahalu amebainisha kuwa, suala la Maadili katika Jamii ni zito na hakuna ubishi kwamba Jamii kwa jamii hivyo UB imeona ni vyema siku za usoni ianzishe Taasisi ya Maadili ambayo itakuwa na masomo hayo kwa wanafunzi wa chuo hicho na wa fani mbalimbali.
” Wakati tunaanzisha UB mwaka 2011,waasisi wa UB tuliona kuwa UB iwe na somo la ” Leadership and Good Governance’. kwasababu tulikuwa tunafahahamu Nchi za Afrika bado zinakabiliwa na tatizo la viongozi bora , hivyo tukaanzisha somo hilo ambalo nilazima mwanafunzi anayesoma UB wa ngazi yoyote asome hilo somo ambalo linamsaidia mwanafunzi kutambua kiongozi mahali popote pale aweje, mambo gani afanye na yapi asifanye .
Ameongeza kuwa, tayari mchakato wa kuanzisha Taasisi hiyo unaendelea na upo katika hatua nzuri na pindi utakapokamilika, wataufahamisha umma na Jamii ya wasomi wa chuo hicho.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Kozi ya ‘Leadership and Good Governance ‘ , Dk. Asia Mwanzi alisema lengo la mashindano hayo yaliyofadhiliwa na Taasisi ya FAHAMU ni kuwajengea wanafunzi wa chuo hicho uwezo wa kukaa chini na kuandika mambo mbalimbali yanayohusu Jamii yao bila woga ili mamlaka husika iweze kuyafanyia kazi mawazo yao .
Katika tukio hilo, mshindi wa kwanza, alikabidhiwa tuzo na dola za Kimarekani 100 na vitabu ambapo mshindi huyo ni Mwanafunzi Baraka Samuel.
Baraka alishukuru kwa ushindi huo, kwani ameeleza kuwa, washiriki walikuwa ni wengi lakini Insha yake ikaibuka kuwa mshindi.
Akizungumzia juu ya Insha yake hiyo, Baraka alisema aliandika kuhusu sera Taasisi ya Vyuo Vikuu ( TCU) ya kuinua viwango vya kudahili wanafunzi wanaojiunga kujiunga na Vyuo vikuu nchini ambapo ameshauri TCU na serikali kwanza iboreshe elimu za Msingi na Sekondari ikishafanikiwa katika ngazi hizo ndiyo ije iongeze viwango vya udahili wa wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu.
Mshindi wa pili katika tukio hilo, mshindi alikuwa Mwanafunzi wa Shahada ya pili ya Sheria ambaye pia ni Wakili wa Serikali,Frola Massawe ambaye naye amepewa tuzo.
Imetolewa na Ofisa Habari wa UB, Happiness Katabazi

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu, Profesa Costa Mahalu
Sign up here with your email
