BANA MATUMIZI YAKWAMISHA KESI - Rhevan Media

BANA MATUMIZI YAKWAMISHA KESI



Moshi. Utaratibu wa kubana matumizi nchini unaonekana kuutikisa mhimili wa Mahakama, baada ya kesi za mauaji kushindwa kuendeshwa nje ya mji wa Moshi.
Mwaka jana, vikao vya kesi za mauaji vilikuwa vifanyikie wilayani Rombo kati ya Novemba 14 na Desemba, Hai ilikuwa Septemba 26 hadi Oktoba 20 na Same kati ya Mei 23 na Juni 24.
Hata hivyo, vikao hivyo havikufanyika kutokana na ufinyu wa bajeti unaoukabili mhimili huo, huku kukiwa na dalili hali hiyo kujirudia mwaka huu.
Habari za uhakika kutoka kwa mawakili wa kujitegemea, zimeeleza kuwa hali hiyo imechangiwa na Serikali kuipa Mahakama fedha kidogo kulingana na bajeti halisi.
Wakili Youngsaviour Msuya alisema licha ya Serikali kuwa na vipaumbele vyake, mhimili wa Mahakama ni muhimu katika kusimamia utulivu wa nchi. “Unajua kunapotokea mauaji wananchi wanaweza kusema huyu kaua lakini yeye akakataa. Kesi zikizikilizwa kwa wakati na hukumu kutolewa, inaepusha visasi kwa jamii,” alisema Msuya.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) tawi la Moshi, David Shilatu alisema taarifa walizonazo ni kuwa Mahakama haina fedha za kutosha kujiendesha kwa ufanisi. “Session (vikao) vilivyokuwa vifanyike Rombo, Hai na Same hazitafanyika isipokuwa hapa Moshi tu. Mahakama haina pesa za kuwalipa ile fee (ada) mawakili wa kujitegemea,” alisema.
Shilatu alisema utaratibu ni kuwa Mahakama humlipa Sh60,000 kwa siku kila wakili aneyeteuliwa kumtetea bure mshtakiwa wa mauaji, lakini bajeti hiyo imekwama.
Wakili mwingine, Julius Semali alisema anachokiona ni kwamba Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa majengo, lakini siyo matumizi ya kawaida.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Bernard Mpepo alikiri kuwapo kwa tatizo la fedha na kwamba, hilo limewasababisha kuendesha kesi zote za mauaji Moshi.
“Hilo tatizo lipo, kwa hiyo tunapanga kesi za hapa mjini ili kuepuka gharama za kwenda nje ya Moshi zikiwamo za mawakili wa kujitegemea. Tunapanga kesi ambazo ziko ndani ya uwezo wetu,” alisema.

Previous
Next Post »