Jeshi
la Polisi nchini limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa utapeli
anayejulikana kwa jina la Wilfred Masawe (36) , mkazi wa Buza, Temeke
jijini Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi Mtuhumiwa huyo
alikuwa akitumia mbinu mbalimbali kutapeli zikiwemo kujitambulisha kama
kiongozi wa serikali kwa kutumia mtandao wa Whatsapp, huku akieleza
kuwa yupo nje ya nchi na kuna tatizo la msiba ambao umetokea nchini na
unamuhusu na hivyo alikua akitoa maelekezo kwa watendaji wa serikali
waweze kusaidia gharama za matibabu hospitalini, gharama za kusafirisha
mwili wa marehemu na gharama za mazishi.
Taarifa
hiyo pia imesema mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu ya kujifanya
kiongozi mkubwa wa dini ya kikristo (Askofu) na kuwaambia waumini na
viongozi mbalimbali kuhusu maandalizi ya makongamano ya kidini kwa lengo
la kuwaomba michango kuweza kufanikisha makongamano hayo.
Baadhi
ya matukio aliyofanikiwa kutapeli ni pamoja na kuwatapeli viongozi wa
serikali, wafanyabiashara, mameneja na wakurugenzi wa taasisi za umma,
wanasiasa pamoja na waumini wa madhehebu ya dini.
Aidha,
matukio yote hayo alikuwa akiyafanya peke yake na alikuwa akiyaendesha
kwa mawasiliano ya njia ya ujumbe mfupi (SMS) bila kuzungumza kwa simu.
Jeshi la Polisi linakamilisha taratibu za kisheria ili mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
***
Sign up here with your email