WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda tume kuchunguza taarifa inayoelezea utaratibu
uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa
Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti Serengeti pamoja na
kutafuta kaburi la faru huyo.
Amesema
timu hiyo ya wataalamu tayari imeshafika Sasakwa VIP Grumet kwa ajili ya kutafuta
kaburi na kuchukua vinasaba vya masalia ya faru John na kisha watakwenda kwenye
Hifadhi ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wake na kuvilinganisha na pembe hiyo ili kubaini kama kweli pembe aliyopelekewa ni
ya faru John au laa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Desemba 18, 2016) wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha. Ziara hiyo ililenga
kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuona utoaji wa huduma kwa
wananchi.
"Tume
niliyounda kwa ajili ya uchunguzi wa faru John imetua VIP Grumet
Serengeti kujiridhisha kama kuna kaburi la faru John na kama lipo wachukue vinasaba
na baada ya hapo watakwenda Creter na kuchukua vinasaba vya watoto wa faru John
na kuvipima kwa pamoja. Lengo ni kutaka kubaini kama pembe iliyowasilishwa
kwangu Disemba 9 mwaka huu ni ya faru John,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema wakati faru John akiwa V I P Grumet taarifa zilisema ni mgonjwa na
daktari alipompima mara ya kwanza akabaini faru huyo hakuna na ugonjwa wowote.”Daktari
alimpima tena kwa mara ya pili taarifa zikasema tena si mgonjwa ghafla wakasema amekufa. Hili haliwezekani,”.
Waziri
Mkuu amesema ameiagiza timu hiyo kufanya kazi ya uchunguzi wa taarifa hizo kikamilifu
kwa sababu Serikali imetumia fedha nyingi kuwaleta faru hao kutoka nchini
Afrika Kusini. Ni lazima nyara hizo za Serikali zilindwe kwa manufaa Taifa.
Waziri Mkuu
alipokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka
Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye
Hifadhi ya Grumeti Desemba 9, 2016 katika kikao kilichofanyika kwenye makazi ya
Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho
kilihudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na
baadhi ya watendaji wa wizara yake, Baada ya kupokea taarifa hiyo Waziri Mkuu alisema
taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.Akisoma
taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema hadi kufikia Desemba
2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2)
ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
“Kati ya
faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia
70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa
faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,”
alisema Waziri Maghembe. Baada
ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru
John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu.
Taarifa hiyo
iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru. Kamati hiyo inaundwa
na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa
NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Akikabidhi
pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo
cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande alimweleza kwamba
pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na
uzito wa kilo 2.3.
Desemba 6,
mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika
kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo
Alhamisi, Desemba 8.
Alitoa agizo
hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro,
mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa
Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 18, 2016.
Sign up here with your email