UPEPO WABADILIKA BEI YA KOROSHO - Rhevan Media

UPEPO WABADILIKA BEI YA KOROSHO

Tokeo la picha la korosho mtwara
BAADA ya neema ya kupanda kwa bei ya korosho kulikotajwa kunufaisha wakulima wengi wa zao hilo, hasa katika mikoa ya Kusini ambako baadhi ya wakulima walibadilisha ghafla staili zao za maisha, Serikali imekiri kuwa bei ya zao hilo imeanza kushuka sokoni kutoka Sh 4,000 hadi kufikia Sh 3,000 kwa kilo.
Imeeleza kuwa, miongoni mwa sababu zilizochangia kushuka kwa bei ya korosho ni ushindani wa soko. Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba wakati akizungumzia maendeleo ya kilimo cha korosho.
Alisema pamoja na kwamba wakulima wa zao hilo kwa sasa wanaendelea kunufaika na kupanda kwa bei ya zao hilo, hali inaanza kubadilika kutokana na ushindani wa zao hilo katika masoko mbalimbali kuongezeka.
Alitaja sababu za kushuka kwa bei hiyo kuwa ni pamoja na nchi nyingine zinazozalisha korosho masoko yao kuwa yamefufuliwa na hivyo kuifanya Tanzania isiwe nchi pekee inayozalisha na kusambaza korosho.
Alisema wakati Tanzania ikiimarisha uzalishaji na soko la zao hilo, nchi kama Thailand, Msumbiji na nyingine za Afrika Magharibi zilikuwa hazijafungua masoko yao, lakini kwa sasa nchi hizo zote zimefungua masoko yao na hivyo kuiongezea ushindani Tanzania.
Aidha, alisema sababu nyingine ni wafanyabiashara nchini kupata ugumu katika mfumo mzima wa mzunguko wa uuzaji na uuzaji wa zao hilo kwa haraka, hali inayosababisha ushindani kupungua.
Alisema mwanzoni kulikuwa na kampuni 118 zilisajiliwa kununua korosho na jinsi msimu wa korosho unavyosonga mbele kampuni hizo zimeendelea kushuka.
Hata hivyo, alisema Serikali imeanza kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali kama ilivyokuwa kwa bei ya zao hilo mwaka jana ambapo baada ya kurekebishwa kwa baadhi ya kanuni zilizokuwepo kwenye bodi ya utoaji wa leseni, mafanikio yameanza kuonekana kwa kupunguza masharti ya leseni na hivyo kupaisha bei kufikia Sh 2,900 mwaka jana na kuna wakati ilipanda hadi Sh 4,000 kwa kilo.
Alisema kwa sasa bei ya ununuaji wa korosho kwa kilo imefikia Sh 3,700 kiwango ambacho kiuhalisia bado ni mafanikio makubwa kwa sekta hiyo ya zao la korosho. Alisema wizara hiyo imejipanga kuhakikisha inachukua hatua za kulinda mafanikio hayo ili kuzuia bei na zao hilo la korosho lisiporomoke.
Previous
Next Post »