SAKATA la kupotea ghafla kwa aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bernard Saanane, limechukua sura mpya, baada ya familia yake kumjia juu mwajiri wake, Chadema, kwa kile inachodai chama hicho kimeshindwa kuonyesha dhamira ya dhati ya kumtafuta.
Akizungumza na MTANZANIA jana, baba mzazi wa Saanane, Focus Saanane, alisema anashangazwa na hatua ya Chadema kushindwa kujitokeza hadharani kumtafuta mwanae ambaye amepotea katika mazingira ya kutatanisha.
“Tangu mwanangu Ben amepotea, hatujawahi kumuona (Freeman) Mbowe ambaye ndiye mwajiri wake kama amechukua hatua yoyote ya kukutana na familia yangu, tukashauriana namna ya kumtafuta. Ukimya huu umenistajabisha mno.
“Nilitegemea angekuwa mtu wa kwanza kuja kwangu, tuone njia gani ambayo tunaweza kutumia kumpata Ben. Naumia mno ndugu yangu,” alisema Focus.
Alimtaka Mbowe ajitokeze na kuipa familia taarifa za mahali alipo Ben, kwani wao wametawaliwa na hofu kubwa kutokana na kijana wao kutoweka akiwa mikononi mwake.
“Ninamtaka Mbowe aniletee mwanangu Ben akiwa mzima, nashindwa kujua yupo wapi na nini kinaendelea mpaka sasa kati yake na Ben, haiwezekani mwajiri ashindwe kujua mfanyakazi wake alipo mpaka sasa… bado haliniingii akilini mwangu… suala hili halileti taswira nzuri kwa jamii kama anaendelea kukaa kimya na hazungumzi chochote, si haki,” alisema.
Akizungumza kwa jazba, Focus aliiomba Serikali na vyombo vyake vya dola isaidie kumtafuta Ben kwa nguvu zote kutokana na juhudi za familia kugonga mwamba.
Pia alikanusha vikali taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari, kuwa Ben amefariki dunia. Kwamba familia yake imeitwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwenda kutambua maiti moja iliyochomwa moto maeneo ya Uru Ongoma. Kata ya Uru Kaskazini wilayani Moshi.
CHADEMA
Akijibu malalamiko hayo, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alisema si kweli kama Mbowe ameamua kukaa kimya, bali wao wameiachia Serikali kufanya uchunguzi wa kina na kutoa taarifa.
“Wakati jambo hili linatokea, mwenyekiti wetu (Mbowe) alikuwa nje ya nchi, naelewa presha aliyonayo mzazi wa Ben katika suala hili, tunaendelea kuhangaika nalo na kutaka vyombo vya dola vichukue hatua.
“Tunaitaka Serikali ifanyie kazi mambo matatu ambayo yako ndani ya uwezo wake, iseme wapi alipo Ben, mara ya mwisho aliongea kwa simu yake na nani na wapi na itumie kila aina ya uwezo wa kumleta kwa sababu si mtuhumiwa,” alisema Makene.
RPC
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana, kuwa uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo kuhusu mwili uliookotwa eneo la Uru Ogoma, si wa Ben kama ambavyo iliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
“Uchunguzi uliofanywa umebaini aliyefariki ni Steven Kimario (55), mkazi wa Sanya Juu wilayani Siha, ambaye aliuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira, baada ya kukutwa akifanya jaribio la kubaka mtoto wa dada yake mwenye umri wa miaka tisa.
Sign up here with your email