KWA takribani wiki moja sasa nimekuwa katika maeneo tofauti ya mikoa ya Arusha na Mara, kufuatilia suala la mnyamapori Faru John, ambaye awali alidaiwa kuuzwa kwa mwekezaji wa Kampuni ya Grumeti.
Mjadala wa Faru John uliibuliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Desemba 6, mwaka huu alipokuwa katika ziara ya kikazi wilayani Ngorongoro, Arusha.
Wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Majaliwa, alisema ndani ya mamlaka hayo kuna vitendo vya rushwa, na kwamba Faru John alihamishwa na kupelekwa Grumeti, Serengeti mkoani Mara, baada ya baadhi ya wafanyakazi kupewa Sh milioni 100 na kuahidiwa Sh milioni 100 zingine zilizokuwa hazijatoka.
Pia aliagiza apewe nyaraka zote zinazohusiana na mchakato wa kumhamisha mnyamapori huyo, zikiwamo taarifa za madaktari na akaagiza ifikapo Desemba 8, mwaka huu awe amezipata pamoja na pembe za Faru John.
Wahusika walitimiza matakwa ya Majaliwa kwa kumpelekea nyaraka pamoja na pembe za Faru John, na baada ya hapo vyombo vya dola vimekuwa vikiendelea na uchunguzi katika ngazi mbalimbali.
Lakini Majaliwa hakuishia hapo tu, alinukuliwa akisema kuwa hata Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alifichwa kuhusu kuhamishwa kwa Faru John, ingawaje wakati anahamishwa Desemba 8, mwaka juzi, Waziri wa wizara hiyo alikuwa ni Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu alikuwa Mizengo Pinda.
Kwa hiyo si Majaliwa wala Profesa Maghembe waliokuwa katika nyadhifa walizonazo sasa wakati mchakato halali wa kumhamisha Faru John ukiendelea.
Kama ilivyobainishwa awali, katika kufuatilia suala hili nyeti nimefanikiwa kukutana na kuzungumza na wadau mbalimbali, pamoja na kuona nyaraka nyingi kuhusiana na kuhamishwa kwa Faru John. Nyaraka tutakazozichapa na kuzijadili katika makala zijazo kuhusu Faru John.
Naweza kusema bila shaka yoyote kuwa, mchakato wa kumhamisha Faru John ni halali kabisa, ulifuata taratibu zote za kiserikali na kitaalamu, na mazingira ya kuhamishwa kwake tangu awali hayatoi mwanya wowote ule wa kuwapo vitendo vya rushwa.
Pia Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa taratibu za kuwahamisha faru kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni taratibu za kawaida kabisa, na zimekuwa zikifanyika kwa miaka mingi, kwa hiyo kuhamishwa kwa Faru John kutoka Ngorongoro kwenda Grumeti halikuwa jambo jipya au la ajabu, kiasi cha kusababisha nchi nzima ihamaki.
Mwaka 2010 Tanzania ilipokea faru watano kutoka Afrika Kusini ambao wapo Hifadhi ya Taifa Serengeti, ingawaje majangili waliwaua 2 kati yao, hata Grumeti kuna faru wengine walitoka Uingereza miaka kadhaa iliyopita, hii ni mifano michache kuonyesha uhamishaji wa faru si kosa, ni jambo la kawaida.
Lakini baada ya Majaliwa kukabidhiwa pembe na nyaraka husika, habari za uongo na uzushi zikazagaa kwamba zile pembe si za Faru John, lengo la upotoshaji huo likiwa kuuaminisha umma wa Watanzania kuwa pembe zake ziliuzwa.
Ni uvumi na uongo huo ndio ulimfanya Majaliwa aagize kaburi la Faru John likafukuliwe, ingawaje katika miaka isiyopungua 10 ambayo nimekuwa nikitafuta habari na makala kuhusu masuala ya uhifadhi, sijawahi kuona kaburi au makaburi ya wanyamapori, ambacho huwa nakiona ni mizoga na mifupa.
Pia Majaliwa aliagiza vifanyike vipimo vya vinasaba (DNA) vikihusisha mabaki ya Faru John, pembe na watoto wake waliopo Ngorongoro, watoto wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 25. Ndani ya Ngorongoro kuna faru zaidi ya 50 kwa sasa.
Baada ya kueneo uongo kuwa pembe alizopewa Majaliwa si za Faru John, nilistuka, nikawasiliana na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk. Fadhili Manongi, ambapo kwa kujiamini na bila kung’ata maneno alisema pembe zile ni za John
“Nina uhakika kwa asilimia 100 kuwa zile ni pembe za John, pia ni kweli sisi ndio tuliikata ile ya mbele, ili kupunguza madhara pindi anapopigana na faru wengine, hata kipande tulichokata kipo ofisini,” anasema Dk. Manongi.
Pembe alizokabidhiwa Majaliwa mojawapo imewekwa kifaa maalumu cha utambuzi kijulikanacho kama ‘transponder’, kifaa ambacho kikitolewa ndani ya pembe na kuwekwa betri, kitatoa taarifa kuthibitisha kama ile pembe ni ya Faru John au la? Hakuna sababu ya kupoteza muda na fedha kufanya vipimo vya vinasaba.
Tuhuma za kutolewa kwa rushwa ya Sh milioni 100 kwa watumishi wa Ngorongoro si tuhuma ndogo, hivyo kama haitathibitika, basi ni jambo la kiungwana kabisa itolewe kauli nyingine kufuta ile ya awali kwa utaratibu utaoonekana unafaa.
Haiingii akilini kwamba mwekezaji Grumeti atoe fedha ili kumtorosha Faru John, wakati huyo huyo mmiliki wa Grumeti Bilionea wa Marekani, Paul Tudo Jones, amekuwa akituletea faru kutoka nje kwa gharama zake mwenyewe, ambapo gharama ya kumsafirisha faru mmoja kutoka Ulaya hadi Tanzania ni zaidi ya Sh milioni 200.
Pia ifahamike kuwa, kwa mujibu wa sheria na taratibu wa wanyamapori Tanzania, faru yoyote anayekanyaga ardhi ya Tanzania, hugeuka na kuwa mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Kwa faru ambao Grumeti amekuwa akiwaleta Tanzania wanakuwa mali yetu na si wa kwake tena.
Sasa ukiliangalia sakata zima la Faru John, utagundua kuna nia ovu ndani yake, kwa sababu kwanini mtu atoe taarifa za uongo na kufikia hatua ya kumpotosha Majaliwa ambaye ni kiongozi mkubwa katika nchi.
Kwa taarifa zilizopo hadi sasa, nashauri vyombo vya dola viache kupoteza muda kuhoji watendaji wa Tanapa, Ngorongoro, Tawira na wizara na badala yake washughulike na mtoa taarifa, kwa sababu alitoa taarifa ilhali akijua anadandanya.
Sidhani kama ni sahihi kwa mtu kukosa ‘tip’, halafu kujenga chuki dhidi ya wenzake waliobahatika kupata ‘tip’ baada ya kazi, kisha unakaa chini na kutumia nafasi uliyonayo inayokuwezesha kufikisha taarifa unayotaka ngazi za juu kuwamaliza wenzio, kwa kutoa taarifa za uongo.
Sakata la Faru John lisiishe kimyakimya, lazima mwisho wake ufahamike na uwekwe hadharani, na kama kuna mpotoshaji ambaye naamini kabisa yupo, basi achukuliwe hatua stahiki, ili tukio baya kama hili lisitokee tena.
Sign up here with your email