Katibu
wa Mfuko wa Jimbo la Musoma Vijijini na Afisa Mipango wa Wilaya ya
Musoma, Mukama Rugina (aliyesimama) akizungumza wakati wa mkutano wa
kujadili matumizi ya fedha za mfuko huo.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya
Tegeruka, Musoma Vijijini waliohudhuria mkutano wa kujadili matumizi ya
fedha za Mfuko wa Jimbo hilo.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini
na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia)
akizungumza jambo wakati wa mkutano wa kujadili matumizi ya fedha za
Mfuko wa Jimbo. Kushoto ni wajumbe wa Kamati ya Mfuko wa Jimbo la Musoma
Vijijini.
Diwani wa Kata ya Tegeruka,
Benjamin Maheke (aliyesimama) akizungumza wakati wa mkutano wa kujadili
matumizi ya fedha za mfuko wa Jimbo la Musoma Vijijini.
……………….
Wajumbe wa Kamati ya Mfuko wa
Jimbo la Musoma Vijijini wameagizwa kuhakikisha wanakagua utekelezaji wa
miradi ya kilimo ya vikundi vilivyokabidhiwa vifaa kutoka kwenye mfuko
huo ili kujiridhisha.
Agizo hilo limetolewa hivi
karibuni na Mbunge wa Jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati husika wakati wa mkutano wa hadhara wa kuainisha
matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo kwa Awamu ya Pili uliofanyika katika
kijiji cha Tegeruka, Musoma Vijijini.
Ilielezwa kwamba Awamu ya kwanza
ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya Mfuko wa Jimbo hilo ni shilingi
milioni 70,820,000 ambazo zilitumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo
shilingi milioni 20,000,000 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Murangi.
Fedha zingine ni milioni
27,500,000 ambazo zilitumika kwa ajili ya kurekebisha nyumba na madarasa
yaliyokuwa yameezuliwa na upepo kwa shule mbili za msingi, milioni
22,500,000 ilitumika kununulia mashine za umwagiliaji, mbegu za
mbogamboga na matunda pamoja na dawa za kilimo na shilingi 820,000
zilitengwa kwa ajili ya kuwezesha ufuatiliaji.
Profesa Muhongo alisema ni jukumu
la Kamati husika kuhakikisha fedha imetumika kwa matumizi yaliyokubaliwa
na aliagiza vikundi vyenye miradi ya kilimo ambayo haijaanza
vinyang’anywe vifaa vilivyokabidhiwa na vipewe vikundi vingine vyenye
vyenye nia dhabiti ya kuendeleza kilomo.
“Tembeleeni hivi vikundi, mkikuta
havijaanza kutumia vifaa tulivyowapatia mvinyanga’anye na vifaa hivyo
vigawiwe kwenye vikundi vyenye nia ya dhati,” aliagiza Profesa Muhongo.
Akizungumzia Awamu ya Pili ya
Mfuko wa Jimbo, Profesa Muhongo alisema Mfuko wa Jimbo umepokea kiasi
cha shilingi milioni 38,479,000 ambazo alisema Kamati husika kwa
kushirikiana na wananchi pamoja na madiwani wamependekeza zitumike kwa
ajili ya kuboresha kilimo.
Alisema shilingi milioni
16,000,000 zitatumika kwa ajili ya kununulia mbegu za kisasa za mihogo
za mkombozi kiasi cha vipando 532,000 ambazo zitagawiwa kwenye Kata 21
kwa ajili ya vijiji 68, na shilingi milioni 21,900,000 itatumika
kununulia mashine 21 za kukamulia alizeti.
Aliongeza kuwa hapo awali
alisambaza mbegu za alizeti za majaribio kiasi cha kilo 4000 ambazo
alisema zimeonesha mafanikio na hivyo aliongeza mbegu zilizoboreshwa
kutoka Arusha kiasi cha kilo 5000 ambazo pia zilisambazwa.
Alisema ili kujiongezea kipato
kutokana na kilimo cha alizeti, wameamua badala ya kuuza mbegu, wakulima
hao watauza mafuta na ndiyo sababu ya kutenga kiasi hicho cha fedha kwa
ajili ya mashine hizo ambazo alizielezea kuwa ni za kuzungusha kwa
mikono na hazihitaji mafuta wala umeme.
“Hizi nilitoa fedha yangu na sio katika mfuko wa jimbo; na kukitokea mapungufu nifahamisheni nijazilizie,” alisema.
Akizungumzia utaratibu wa mashine
hizo, alisema kila Kata itakabidhiwa mashine yake na kwamba zitafungwa
kwenye ofisi za kata chini ya usimamizi wa Afisa kilimo.
Sign up here with your email