KAMANDA
wa Brigedi ya Nyuki ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
Brigedia Jenerali Cyril Mhaiki, amefariki dunia katika Hospitali ya
Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika
salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
Tanzania, Davis Mwamunyange, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, alisema jana kuwa, amepokea kwa huzuni
kubwa taarifa za kifo cha Brigedia Jenerali Mhaiki aliyefikwa na mauti
juzi.
Dk
Shein kwa niaba yake na ya wananchi wote Zanzibar, alisema wamepokea
kwa mshtuko, taarifa ya kifo cha Kamanda huyo hodari aliyetoa mchango
mkubwa katika shughuli za ulinzi na usalama na maendeleo ya nchi.
Aidha,
salamu hizo za rambirambi zilieleza kuwa Brigedia Jenerali Mhaiki
ameacha pengo kubwa, si tu kwa familia yake, bali kwa Brigedi ya Nyuki,
JWTZ na nchi kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa mchango wake
hautosahaulika.
Alimuomba
Mwamunyange kuzifikisha salamu hizo za rambirambi kwa wanafamilia,
maofisa na wapiganaji wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama.
Pamoja
na hayo, salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira
ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu katika kipindi hiki kigumu cha
msiba huku akimuomba Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema Kamanda huyo.
Sign up here with your email