Uamuzi wa kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata
rufaa dhidi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless
Lema, unatarajiwa kutolewa Desemba 20, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha.
Uamuzi huo utatolewa baada ya Lema jana kufanikiwa kuwasilisha maombi yake ya kuongezewa muda wa kuleta notisi hiyo ya rufaa dhidi ya dhamana yake baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi mbili za mawakili wa Serikali waliokuwa wakitaka maombi hayo yasisikilizwe.
Mbele ya Jaji Dk. Modesta Opiyo wa mahakama hiyo, upande wa Jamhuri
ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Hashim Ngole, Matenus Marandu, Elizabeth
Swai na Adelaide Kasala huku Lema akitetewa na Wakili Sheck Mfinanga na
Faraji Mangula.
Katika maombi hayo namba 69 ya mwaka huu, baada ya kusikiliza hoja za
pande zote mbili, Jaji Dk. Opiyo alisema kuwa atatoa uamuzi huo siku
hiyo saa sita mchana.
“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote nitatoa uamuzi Jumanne ijayo
saa sita mchana, msije asubuhi ili nipate muda wa kupitia hoja zenu,”
alisema Jaji Dk. Opiyo.
Awali, akitoa uamuzi wa pingamizi mbili zilizotolewa Desemba 14,
mwaka huu na mawakili hao wa Jamhuri, Jaji Dk. Opiyo, aliyesoma uamuzi
huo kwa muda wa dakika 50 kuanzia saa 5:30 asubuhi hadi saa 6:20 mchana,
alisema ameamua kuzitupa pingamizi hizo baada ya kuziona hazina mashiko
ya kisheria.
Alisema kuwa hakuna maombi kama hayo yaliyoacha kusikilizwa
mahakamani kwa kushindwa kuonyesha kifungu namba 392 A cha sheria ya
uendeshaji wa mashauri ya jinai hivyo akalitupa pingamizi la kwanza la
mawakili wa Serikali waliodai maombi hayo hayakufuata utaratibu wa
kisheria ikiwemo kutoonyesha vifungu vya sheria waliyoitumia kuleta
maombi hayo.
“Baada ya kupitia hoja za pande zote, mahakama imeamua kutupa
pingamizi hizo za Jamhuri baada ya kuziona kuwa hazina mashiko kisheria
na hata upande wa Jamhuri ulishindwa kurejea shauri lolote ambalo
limewahi kufanyiwa uamuzi na mahakama za juu kuhusu suala hilo,” alisema
Jaji Dk. Opiyo.
Akizungumzia hoja ya pili ambayo Jamhuri ilidai ya kiapo kinachounga
mkono maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo kimekosewa hivyo hakifai
kwa sababu wamejumuisha mambo yasiyotakiwa kisheria ikiwemo maoni,
mabishano na hitimisho na kubeba hoja za rufaa alisema mahakama hiyo
imeondoa aya ya 11 na 12.
Alisema kuwa aya nyingine za 9, 10, 13 na ile ya 17 zitabaki katika
hati hiyo ya kiapo kwa sababu hazibebi hoja za rufaa, maoni, mabishano
wala hitimisho hivyo mahakama hiyo haiwezi kukataa hati hiyo ya kiapo
iliyoambatanishwa na maombi hayo.
Akiwasilisha hoja za maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi
hiyo ili rufaa hiyo iweze kusikilizwa, Wakili Mfinanga, alidai
mahakamani hapo kuwa maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo chini ya
kifungu 361(2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Alidai kuwa uamuzi wanaotarajia kukatia rufaa ni uliotolewa Novemba
11, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi
Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi
dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Alitaja sababu mbili za msingi za kukatia uamuzi huo rufaa kuwa ni
kuiomba mahakama hiyo ipitie makosa ya kisheria yaliyofanywa na mahakama
ya chini na kusema kuwa uamuzi huo ulimpa mleta maombi (Lema) dhamana
ila kabla hajapewa masharti ya dhamana upande wa Jamhuri ulitoa notisi
ya nia ya kukata rufaa.
“Kwa msingi huo mahakama ilisema imefungwa mkono na hawawezi
kuendelea na jambo lolote kuhusu suala hilo hata uamuzi wake wa kumpa
dhamana haukuwezwa kutimizwa na mahakama haikueleza upande wowote ambao
haujaridhika na uamuzi huo una haki ya kukata rufaa,” alidai Mfinanga na
kuongeza:
“Kuna vitu muhimu na vitasahihishwa iwapo tutaleta notisi ya nia ya
kukata rufaa na rufaa yenyewe kusikilizwa na mahakama yako ambayo ni
msimamizi wa haki na sheria ikatoa ruksa ili tuweze kusikilizwa na
rekodi ya mahakama ya chini iweze kurekebishwa, ni muhimu mahakama
kuzingatia maombi haya pasipo kuzingatia mambo mengine.”
Huku akirejea mashauri mbalimbali ya mahakama za juu, aliendelea
kueleza mahakama hiyo kuwa mahakama ikishasema imempa mtu haki ya
dhamana lazima itaje masharti ya dhamana.
“Tunaomba mahakama itupatie muda tena mfupi ambao hautazidi hata saa
1:30 kwa ajili ya kuleta notisi hiyo ili mahakama iweze kurekebisha
makosa hayo,” alisema.
Akiwasilisha hoja ya pili, Wakili Mangula, alidai mahakamani hapo
kuwa tangu kutolewa kwa uamuzi huo hawajapumzika na muda wote walikuwa
mahakamani.
Alidai kuwa walikuwa wanaenda mahakamani kwa njia tofauti ili kuiomba mahakama irekebishe makosa hayo ya kisheria.
Alidai kuwa baada ya uamuzi huo kutolewa muda wa kazi ulishaisha na
ilikuwa Ijumaa hivyo Novemba 14, mwaka huu walipeleka barua ya
malalamiko mahakamani hapo na walipoitwa pande zote mbili katika shauri
namba 6 lakini walikumbana na pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa
Serikali.
“Novemba 22, mahakama ilitoa uamuzi na kututaka waleta maombi tukate
rufaa na hapo mleta maombi alipata haki yake ya kukata rufaa ambayo
haikuelezwa mahakama ya chini na tulitoa notisi tukiamini tuko ndani ya
muda na hatimaye rufaa ililetwa mbele ya Jaji Mfawidhi Fatuma Masengi,”
alidai.
Alieleza mahakama hiyo kuwa katika rufaa hiyo namba 113, walikutana
tena na pingamizi la Serikali kuwa wametoa notisi ya rufaa hiyo nje ya
muda wa siku moja hivyo hizo ni jitihada walizokuwa wakifanya na si
wazembe, wajinga wa sheria kama ilivyodaiwa na wakili wa Serikali.
Akijibu hoja za waleta maombi hao, Wakili Ngole, alidai kuwa ni
wazembe, wajinga wa sheria na kuwa hata uamuzi wanaolalamikia mahakamani
hapo ambao awali ulimpa mleta maombi dhamana, lakini kabla hajapewa
masharti ya dhamana mahakama iliingiliwa mamlaka yake hawajawasilisha na
maombi hayo.
Wakili huyo alidai mahakamani hapo kuwa hakukuwa na makosa yoyote ya
kisheria kama inavyodaiwa na waleta maombi hao na kudai kuwa baada ya
hakimu kusema mahakama inampa mshtakiwa dhamana Jamhuri kwa haki yake
walisimama na kuifahamisha mahakama wana nia ya kukata rufaa.
“Ni utaratibu wa kisheria kuwa panapokuwa na notisi ya nia ya kukata
rufaa mahakama haiwezi kuendelea na jambo lolote kuhusiana na kesi hiyo,
hivyo hakimu asingeweza kuendelea na kesi na inafahamika notisi
inasimama badala ya rufaa,” alidai na kuongeza:
“Kwa mujibu wa kifungu 359(1) na 361(1) cha sheria ya mwenendo wa
makosa ya jinai, vinaeleza mtu ambaye hajaridhika na hatua yoyote au
uamuzi uliotolewa au kupitishwa anaweza kukata rufaa mahakama za juu.”
Lema anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika mahabusu ya Gereza
Kuu la Kisongo baada ya kukamatwa Novemba 2, mwaka huu nje ya Viwanja
vya Bunge mjini Dodoma ambapo alifikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka
huu akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. Magufuli.
Sign up here with your email