HABARI HIVI PUNDE : WAZIRI AAMURU DIWANI AKAMATWE - Rhevan Media

HABARI HIVI PUNDE : WAZIRI AAMURU DIWANI AKAMATWE

Tokeo la picha la WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Gerson LwengeWAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge ameagiza kukamatwa kwa Diwani wa Kata ya Lusaka iliyo katika wilaya ya Sumbawanga, Ameir Nkurlu (Chadema) ambaye anatuhumiwa kuwahamasisha wananchi kuvamia na mkulima katika vyanzo vya maji.
Ameagiza kwamba, ili Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfani Haule aendelee kujihakikishia kuwepo katika nafasi hiyo, atumie nguvu zote kuwaondoa wavamizi wote walioshawishiwa na diwani huyo kulima kwenye vyanzo vya maji na kusababisha uharibifu wa mazingira.
Waziri Lwenge ametoa agizo hilo katika mji mdogo wa Laela wilayani Sumbawanga, muda mfupi baada ya kukagua na kupokea taarifa ya mradi wa maji wa Kikundi cha Lael, awamu ya kwanza na ya pili na kuweka jiwe la msingi.
Alipotembelea na kukagua mradi huo katika kijiji cha Kizumbi alishuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira uliofanywa na wananchi wanaofanya shughuli zao za kibinadamu kwa kukata miti ili kuanzisha mashamba mapya na kulima katika chanzo cha mto.
Lwenge alitaarifiwa kuwa wavamizi hao wameshawishiwa na Diwani wa Kata ya Lusaka kulima kwenye vyanzo vya mito na kusababisha uharibifu mkubwa.
Aliwaagiza Dk Haule na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nyangi Msemakweli kuanzisha kampeni kabambe ya kupanda miti ili pamoja na kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi katika wilaya hiyo.
Akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Kalambo, Waziri Lwenge alielezwa kuwa kamati ya maji ya kijiji cha Mwimbi ambayo inadaiwa kuanzishwa bila kufuata utaratibu mwezi mmoja uliopita kuwa ni hewa.
Lwenge alimpatia miezi miwili Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Simon Ngagani kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa katika kijiji cha Mwimbi unafungiwa vifaa vinavyotumia nishati ya jua ili wakazi wake waanze kupata huduma ya maji safi na salama. Pia amewaagiza mkurugenzi huyo kuhakikisha kamati ya maji katika kijiji hicho cha Mwimbi inaundwa na kujengewa uwezo.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji katika kijiji cha Mwimbi, Ngagani alisema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 300 umeshindwa kutoa huduma kwa wananchi kwa zaidi ya miaka mitatu, kutokana na wananchi kutokuwa na uwezo wa kununua mafuta ya dizeli ya kuendeshea mtambo wa kusukuma maji.
Previous
Next Post »