CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kinatuhumiwa kujimilikisha maeneo ya mabondeni kinyume cha sheria za, kutafutia hati na kulikodisha kwa bei kubwa kwa wafanyabishara wa ABG African Link Traders Ltd kabla ya kuanza kuamriwa na Baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC).
Mmady Aboubakari, Meneja wa ABG, amedaiwa kuwa katika eneo la Buguruni, kiwanja namba 1010 eneo la Sukita, kampuni ya ABG iliingia mkataba tarehe 1 Agosti 2008 na Jitegemee Trading Company ambayo ni kampuni ya kibiashara ya chama hicho kikongwe nchini.Kwa mujibu wa mkataba huo kampuni hiyo mali ya CCM ilimruhusu mwekezaji huyo afukie bonde kwa kujaza kifusi, ajenge ukuta kuzunguka eneo la mita za mraba 50,000,ajenge godauni na majengo mengine kufanikisha kazi za mwekezaji ndani ya miaka mitatu tu.
Aidha kampuni hiyo ya jitegemee ilimwonya mwekezaji huyo uwekezaji wake usizidi dola za kimarekani 880,000.
Mkataba kati ya Kampuni ya kibiashara ya CCM ijulikanayo kama jitegemee na ABG African Link Traders tarehe 1 Agosti 2008.
Hadi mwekezaji huyo anakabidhiwa eneo hilo na kupewa muda wa kukamilisha kazi kwa miaka mitatu, eneo hilo halikuwa na hati, na CCM kama wamiliki walipata hati ya eneo hilo mwaka 2010, miaka miwili baadaye kisha kumkabidhi mwekezaji.
Hata hivyo pamoja na kumpatia hati, CCM hawakumpa ruhusa ya kujenga (Building Permit) ambayo walimpatia miaka miwili baadaye, kuruhusu mwekezaji ajenge jengo la ghorofa mbili, na ukuta kuzunguka eneo hilo.
Hadi wanampatia ruhusa ya kuanza kujenga, CCM ilishakusanya kodi kwa miaka mitatu, na ilikuwa ikilipwa kwa mfumo wa dola za kimarekani, huku mwekezaji huyo akiandikiwa onyo na Baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira kuvunja ukuta aliojenga kwa gharama kubwa kwa maelekezo ya CCM
NEMC iliandikia ABG waraka huo wa kutaka ibomoe ukuta Oktoba 4, 2013 yenye kumb NEMC/04/92/2/VOL.1/30 iliyosainiwa na Ignace Mchalo kwa niaba ya Mkurugenzi wake.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kampuni ya ABG imekuwa ikilipa kodi bila usumbufu isipokuwa baada ya kuamriwa ivunje ukuta huo, CCM wamekuwa wakikataa kulipa gharama za kuvunja ukuta, au kumwongezea mwekezaji huo eneo ili aweze kulipa kodi stahiki ya eneo lisilo na mgogoro.
CCM wametuingiza hasara na bado kwenye gazeti lao wametuandika kuwa tumekuwa wadaiwa sugu jambo ambalo si kweli, anasisitiza Mmady Meneja wa ABG.
“Huu ni utapeli, utakubali vipi kulipa kodi eneo lote wakati NEMC wameshatuandikia barua, NEMC ni taasisi ya serikali ya CCM, na sisi ni wapangaji kwa CCM tumewekeza fedha nyingi lakini tunanyanyaswa.” anasema meneja.
Mmady amesema kampuni ilipewa bonde hilo na Jitegemee ikiwa mali ya CCM alilazimika kununua vifusi vingi vya jiji la Dar es Salaam, vikiwemo vilivyotolewa katika barabara zote wakati wa ujenzi wa mradi wa mwendo kasi.
“Hawa jamaa ni watapeli, nimefukia bonde, nikajenga ukuta, sasa NEMC wanataka nibomoe sababu nimejenga karibu na mto, CCM wakataa wanataka waendelee kulipwa wakati walinionyesha eneo hilo kiutapeli, nimepoteza fedha, sasa nikivunja ni kwa gharama za nani, hawataki kushirikiana.”alisema Mmady
Francis Mafuru, ni meneja mkuu wa kampuni hiyo mali ya CCM, ametafutwa afafanue juu ya sakata hilo kupitia simu yake ya mkononi lakini haikupokelewa. Na alipoandikiwa ujumbe mfupi hakujibu.
Sign up here with your email