Jeshi
la Polisi kupitia msemaji wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi na Msemaji
wa Jeshi hilo, Advera John Bulimba, lilitoa tahadhari za kiusalama
kuhusiana na sikukuu hizo mbele ya waandishi wa habari jana huku pia
wazoefu wa masuala ya biashara na wakuu wa dini wakitoa usia wao
kuhusiana na mambo muhimu ya kuzingatia ili sikukuu isiharibiwe kwa
habari mbaya za misiba na majanga.
Katika
taarifa yao kwa umma, polisi walichimba mkwara mzito kwa kuahidi
kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaofurahia sikukuu hizo kwa
namna inayokiuka sheria na kuhatarisha usalama, huku Askofu Mkuu wa
Jimbo la Mahenge, Agapiti Ndorobo, akionya kuwa kila mmoja anapaswa
kuhakikisha kuwa hatendi mambo ya ovyo na kumchukiza Mungu.
Mhadhiri
wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Joel Silas, aliwashauri
Watanzania kutumia vyema rasilimali zao katika kipindi hiki ili sikukuu
zikimalizika wasibaki bila kitu mikononi mwao.
Keshokutwa,
Watanzania wataungana na watu wengine duniani kote kusherehekea
Krismasi kabla ya kufuatiwa na siku ya kupeana zawadi (Boxing Day)
katika siku inayofuata na mwaka mpya ifikapo mwisho wa mwezi huu.
TAHADHARI YA POLISI
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Bulimba
alisema baadhi ya wahalifu hutumia vipindi vya sikukuu kufanya vitendo
vya kihalifu, lakini akaonya kuwa yeyote atakayejaribu kufanya hivyo
atachukuliwa hatua kali kwa sababu wamejipanga kuhakikisha kuwa amani na
utulivu vinaendelea kudumishwa wakati wote.
“Tumejipanga
vya kutosha, siwezi kuweka mbinu hadharani hapa kwa sababu za
kiusalama, lakini itoshe tu kuwaambia kwamba Jeshi la Polisi liko vizuri
na asithubutu mtu yeyote kufanya uhalifu mahali popote maana tuna mkono
mrefu… tutamkamata,” alisema Bulimba.
Aliwataka
wananchi kutoa ushirikiano kwa kufikisha taarifa haraka wanapobaini
kuwa kuna mtu, kundi au watu wanaowatilia shaka, huku kila mmoja akiwa
mlinzi wa jirani yake katika biashara, makazi na mahali pengine. “Ukiona
kuna mtu anaingia kwa jirani yako halafu humfahamu au unamtilia shaka,
mpigie simu au piga simu polisi kupitia namba 111 na 112,” alisema.
Aliongeza
kuwa jeshi hilo limejipanga pia kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo ya
kuabudia, sehemu za fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine
ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu. Bulimba aliwataka
waendeshaji wa kumbi za starehe kuzingatia uhalali wa matumizi ya kumbi
zao na kuepuka kuzidisha idadi ya watu tofauti na uwezo wa kumbi zao na
kwamba kwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali.
Kuhusu
ulinzi katika barabara, Bulimba alisema jeshi hilo pia limejipanga
kudhibiti matukio ya kizembe ikiwamo madereva walevi na kwamba wameandaa
vituo vya polisi vya kuhamishika ambavyo vitawekwa katika maeneo
tofauti ili kuwarahisishia wananchi kuripoti moja kwa moja matukio
yanayotishia usalama wa raia na mali.
Aidha,
Bulimba alikumbushia vilevile kuwa ni marufuku kusherehekea sikukuu
hizi kwa kupiga fataki, kuchoma matairi barabarani na kuandaa ‘disco
toto’ kwa sababu matendo yote hayo ni uhalifu na wahusika watachukuliwa
hatua za kisheria.
Yafuatayo
ni kati ya mambo mengi ya kuzingatia, yapo takribani tisa ya msingi
kuyakumbuka katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
1. TUMIA FEDHA KWA MPANGO
Kati
ya mambo muhimu ya kuzingatia kuelekea sikukuu ya Krismasi na pia zile
za ‘Boxing Day” na Mwaka Mpya ni kutumia fedha kwa umakini.
Tahadhari
hii inatolewa kutokana na ukweli kuwa baada ya kumalizika kwa sikukuu
hizo, hali huwa ngumu. Isitoshe, Januari ni mwezi unaombatana na
changamoto nyingi. “Kuna masuala ya kodi za pango, ada za watoto shuleni
na majukumu mengine mbalimbali.
Yeyote
yule asipokuwa makini, dunia yote ataiona chungu na Januari ataiona
ndefu. Ni muhimu kukumbuka kuwa kuna maisha baada ya sikukuu hizi,”
mmoja wa wafuatiliaji wa masuala ya kiuchumi aliiambia Nipashe jana.
Akizungumzia
hilo, Dk. Silas alisema ni lazima Watanzania wabadilishe muundo wa
maisha kwa kuelekeza matumizi ya fedha katika mambo ya msingi kwa
kuepuka kuishi kwa mazoea.
2. ZINGATIA SHERIA BARABARANI
Hili
ni eneo jingine la kuchunga sana, hasa kwa madereva na watu wengine
watakaosafiri kutoka eneo moja hadi jingine kwa nia ya kufurahia
sikukuu.
Kwa
mujibu wa Polisi, ajali nyingi zinazotokea katika kipindi cha kuelekea
mwisho wa mwaka husababishwa na watu wanaopuuza sheria za usalama
barabarani, hasa kwa kuendesha vyombo vya moto kwa kasi kubwa na pia
kujazana kwenye vyombo hivyo kupita kiasi.
Wapo
pia wanaotembea kwa miguu barabarani bila ya uangalifu. Ili kutimiza
ndoto ya kuuona mwaka mpya, kila mmoja anapaswa kuzingatia sheria awapo
barabarani.
3. ULEVI KUPITILIZA NI KUITA KIFO
Ulevi
wa pombe kupitiliza kwa baadhi ya madereva ni chanzo kimojawapo kikubwa
cha ajali za mwisho wa mwaka. Baadhi ya ajali hizi zilisababishwa na
ulevi na hivyo, ni muhimu kujua kuwa unywaji holela ni sawa na kujiweka
karibu na kifo au ulemavu wa kudumu.
4. ACHA MICHEPUKO, IPE RAHA FAMILIA
Viongozi
wa dini, akiwamo Askofu Ndorobo, wanasisitiza juu ya upendo kwa
familia, na hasa katika kipindi kama hiki cha kuelekea sikukuu. Kwa
sababu hiyo, inashauriwa kuwa ni vizuri kwa kila mmoja kuachana na
wapenzi wa nje ya ndoa na badala yake kufurahi na familia. Madhara ya
kutenda kinyume chake ni pamoja na kuyumbisha ndoa baada ya sikukuu hizi
kumalizika.
Askofu
Ndorobo alisema ni vyema Watanzania wakajenga utaratibu wa kufurahi kwa
pamoja kwenye matukio ya kifamilia kama kumbukumbu za siku za kuzaliwa,
maisha ya ndoa miaka mitano na zaidi na sherehe nyinginezo, na kwamba
kwa kufanya hivyo yatapunguza maovu mengi kwenye jamii.
5. USILE BATA PEKE YAKO, WAKUMBUKE YATIMA
Inashauriwa
kwa kila mmoja kuwakumbuka yatima, masikini, walemavu na watu wengine
wenye mahitaji maalumu na siyo kufaidi sikukuu na watu wachache wa
familia peke yake. Lengo kubwa katika hili ni pamoja na kusambaza
upendo, kuleta furaha kwa kila mmoja walau katika sikukuu hizi.
6. UMAKINI UNUNUZI WA ZAWADI ZISIWE ‘FEKI’
Mama
au baba wa familia anapokwenda dukani kununulia bidhaa za zawadi kwa
ajili ya sikukuu anapaswa kuwa makini wakati wote kutokana na mrundikano
wa bidhaa bandia katika baadhi ya maeneo. Kwenda kufanya manunuzi
holela kunaweza kuwasababishia kero wapendwa wako badala ya kuwaletea
furaha iliyokusudiwa. Umakini huu uwe maradufu.
7. USIACHE WATOTO PEKE YAO KUOGELEA, DISCO
Kati
ya makosa makubwa hufanyika katika siku za sikukuu ni pamoja na
kuwaachia watoto waende kusherehekea siku hiyo kwenye maeneo mbalimbali
bila ya uangalizi makini. Kwa mfano, ni hatari kuwaachia waogelee peke
yao na pia siyo busara pia kuwaacha warundikane kwenye kumbi za disco,
maarufu kama ‘disco toto’ wakiwa peke yao.
Kutozingatia
maelekezo hayo yaliyosisitizwa jana na Jeshi la Polisi ni sawa na
kujiweka tayari kwa kulia na kusaga meno kutokana na taarifa mbaya
kuhusiana na usalama wa watoto. “Kuna uzembe ambao huwa unafanywa na
wazazi wa kuwaachia watoto kuzurula ovyo na wakati mwingine kuhatarisha
maisha yao.
Sasa
nataka ieleweke hivi, mzazi akibainika amezembea kumlinda mtoto wake na
akaletwa kituoni, lazima atakuwa na kitu cha kujibu na tutamwajibisha,”
alisema Bulimba na kuongeza: “Kwa suala la disco toto, tulishalipiga
marufuku. Halipo kabisa.”
8. EPUKA UCHOMAJI MATAIRI, ULIPUAJI FATAKI
Kusherehekea
sikukuu kwa kuchoma matairi barabarani au kulipua mafataki kiholela ni
miongoni mwa makosa makubwa yanayoweza kuharibu furaha na kuwa kilio kwa
wahusika baada ya kukamatwa na kwenda kuwekwa mahabusu. Bulimba
alilikumbushia hilo jana na kuonya kuwa wakiukaji wa maelekezo hayo
wajiandae kukamatwa na kuwekwa mbaroni.
9. KUMUOGOPA MUNGU
Jambo
lingine muhimu ni kuendeleza amani kwa kufanya matendo yanayozingatia
uwapo wa Mungu. Askofu Ndorobo alisema wapo watu waliozoea uhalifu kwa
kutomhofia Mungu na hilo ni tatizo kubwa linalopaswa kufanyiwa kazi sasa
na hata baada ya kipindi hiki.
“Kinachopungua
kwa (baadhi ya) Watanzania ni hali ya kutomuogopa Mungu kwa dhambi.
Kila Mtanzania ni mlinzi wa mwenzake na pia ni mtunza uhai wa mwenzake.
Ndiyo maana kila mmoja akiheshimu uhai wa mtu… matukio mabaya
hayatatokea,” alisema Askofu Ndorobo.
Sign up here with your email