WANAWAKE wawili wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na
shambulizi lililosababisha kifo cha aliyekuwa Diwani wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Kata ya Igagala, Alexander Pugwi.
Washitakiwa hao, Ashura Jafari na Salma Bakari walidaiwa kutenda kosa
hilo Novemba 12, mwaka huu, katika eneo la Majengo ya Tabora wilayani
Urambo.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya hiyo, Hassan Momba, ilidaiwa
kuwa washitakiwa kwa pamoja siku hiyo, saa 8:00 usiku walimuua Pugwi kwa
kumchoma na kitu chenye ncha kali.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Mkaguzi wa Polisi, Philbert Pimma,
uliiambia mahakama hiyo kuwa washitakiwa hawatakiwi kujibu lolote kwani
shauri lao linapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu, hivyo limepangwa
kutajwa Novemba 29, mwaka huu.
Siku ya tukio, Pungwi ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Igagala inadaiwa
alifika mjini Urambo akitokea kijijini kwake ili kuhudhuria maziko ya
aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta aliyezikwa Jumamosi ya
Novemba 12, mwaka huu.
Sign up here with your email