Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo akiwasalimiana na viongozi wa Wilaya katika eneo la mapokezi wakati wa ziara yake Wilayani hapo.
Nteghenjwa Hosseah , Monduli.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Monduli Mkoani Arusha pamoja na baraza la madiwani la wilaya hiyo kuhakikisha wanabadilisha umiliki wa shamba la Manyara ranch lenye ukubwa wa ekari 44,930 kutoka kwa taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust{TLCT} kwenda kwa wananchi wa vijiji viwili kama Rais wa awamu ya tatu Mhe. Benjamini William Mkapa alivyoagiza.
Rc Gambo alitoa agizo hilo katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kata ya Elesilalei na Makuyuni baada ya kutembelea miradi ya mamilioni ya fedha iliyopo ndani ya shamba hilo inayofadhiliwa na African Wildlife Foundation{AWF} na kuelezwa kero na changamoto zilizopo juu ya umiliki wa shamba hilo kwa taasisi ya TLCT.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha akitoa maelekezo ya kubadilisha Hati ya Umiliki wa shamba kutoka kwa TLCT kwenda kwa wananchi wa vijiji vya Elesilalei na Ortukai.
Alisema nyaraka zinaonyesha wazi kuwa Shamba hilo lilitolewa kwa wananchi wa vijiji vya Elesilalei na Ortukai na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu mwaka 1999 kwa ajili ya kilimo na ufugaji lakini hilo halikufanyika badala yake taasisi ya TLCT ikajimilikisha shamba hilo kinyume na maagizo.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kutokana na hali hiyo ninawaagiza viongozi wote wa wilaya ya Monduli wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na baraza la madiwani kuhakikisha ndani ya muda mfupi wanabadilisha umilikiwa wa shamba hilo kutoka taasisi hiyo kwenda katika vijiji hivyo.
Gambo alisema serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli iko madarakani kwa ajili ya kuwahudumia wanyonge na watu wa hali ya chini na kamwe haiwezi kuona baadhi ya watu fulani wananufaika na rasilimali ya nchi kwa manufaa yao.
Meneja wa Ranch hiyo Ndg. Fidelis Ole Kashe akiwasilisha taarifa ya Shamba hilo kwenye Kikao maalum na Mkuu wa Mkoa wa Arusha pamoja na viongozi wa Wilaya.
Sign up here with your email