Rais Mstaafu wa Cuba Mhe. Fidel Castro enzi za uhai wake
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi
Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Raul Castro kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Cuba
Mhe. Fidel Castro kilichotokea tarehe 25 Novemba, 2016.
Katika Salamu hizo
Rais Magufuli amesema;
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Fidel Castro. Kwa niaba ya Serikali, Wananchi
wa Tanzania na kwa niaba yangu mwenyewe natoa pole nyingi kwako, familia,
Serikali ya Cuba na wananchi wa Cuba kwa kumpoteza mtu muhimu.
Fidel Castro alikuwa kiongozi shupavu wa karne, atakumbukwa
kwa mchango wake mkubwa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na pia kwa
misaada mikubwa aliyoitoa katika kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Alikuwa rafiki wa Tanzania na Afrika nzima, historia ya
Tanzania na Afrika haziwezi kukamilika bila kumtaja Fidel Castro, hakika kifo
chake sio tu ni pigo kwa Cuba bali pia kwa Tanzania na Afrika.
Naungana nawe na wananchi wa Cuba katika kipindi hiki kigumu
cha majonzi, na pia nakuombea kwa Mwenyezi Mungu wewe, familia na wananchi wote
wa Cuba muwe na nguvu, subira na ustahimilivu kutokana na kuondokewa na mpendwa
wenu."
Pia Rais Magufuli
amemuombea marehemu Fidel Castro apumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
26 Novemba,
2016
Sign up here with your email