Imeelezwa
kuwa uchumi wa wananchi wa Mikoa ya Njombe, Mbeya na Ruvuma utaimarika
kwa kasi kama watatumia vizuri fursa ya uwepo wa meli za mizigo na
abiria katika ziwa Nyasa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema kukamilika kwa meli mbili za
mizigo za Mv. Njombe na Mv. Ruvuma na ujenzi wa meli ya abiria ya Mv.
Mbeya ni fursa mpya ya kiuchumi kwa wakazi wa mikoa hiyo.
“Tumejipanga
kuhakikisha tunafungua ukanda huu wa nyanda za juu kusini kiuchumi
hivyo ni jukumu la wananchi kuchangamkia fursa za kibiashara zinazoweza
kusafirishwa ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi”.amesema Eng.
Ngonyani.
Naibu Waziri Ngonyani ameelezea kuridhishwa kwake na
hatua ya ujenzi wa meli za Mv.Njombe na Ruvuma ambao umefikia asilimia
tisini na tisa na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwaamini
makandarasi wazawa wanaofanya kazi kwa ubunifu, uadilifu na uaminifu ili
kutoa fursa nyingi za ajira kwa watanzania.
Kaimu Meneja wa
bandari ya Itungi na Kiwira Eng. Juma Kisavara amemhakikishia Naibu
Waziri Ngonyani kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imejipanga
kuhaikikisha bandari zote kumi na tano zilizopo katika ziwa Nyasa kwa
upande wa Tanzania zinafufuliwa na kutumika kupakia na kushusha mizigi
ikiwemo vifaa vya ujenzi, makaa ya mawe,mbolea na mazao ambayo yana soko
ndani na nchi za jirani.
Eng. Kisavara amemhakishia Naibu wa
Ujenzi kuwa tayari wametafuta soko la kutosha la kusafirisha mizigo
hivyo kuiomba Serikali kuendelea na kasi ya ujenzi wa meli nyingine
zitakazotumika katika ziwa Nyasa.
Zaidi ya shilingi bilioni 11
zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa Meli ya Mv.Ruvuma na Mv. Njombe
zinazojengwa na kampuni ya Songoro Marine Transport ya hapa nchini na
meli hizo zinatarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali mwezi Januari mwakani.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri Ngonyani amekagua ujenzi wa barabara ya
Kikusya-Ipinda hadi Matema KM 34.6 wilayani Kyela inayojengwa kwa
kiwango cha lami na kusisitiza kuwa Serikali italipa fedha kwa
mkandarasi anayejenga barabara hiyo ili kuiwezesha kukamilika kwa muda
uliopangwa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Muonekano wa Meli za
Mv. Njombe na Mv.Ruvuma ambazo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99, meli
hizo zipo katika hatua za majaribio kabla ya kuanza kutoa huduma.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Bw. Salehe Songoro akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (katikati) ripoti ya ukaguzi wa ujenzi wa meli mbili za mizigo katika bandari ya Itungi ziwa Nyasa.
Kaimu Meneja wa bandari ya Itungi na Kiwira Eng. Juma Kisavara (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (katikati) kuhusu namna ya kuondoa mchanga katika kingo za ziwa Nyasa ili kuwezesha meli zinazotengenezwa kuingizwa katika maji kwa urahisi.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akikagua mfumo wa uendeshaji wa Meli ya Mv. Njombe ambao ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99.
Sign up here with your email