Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameendelea kusota katika mahabusu ya
Gereza la Kisongo mjini Arusha akiingiza siku ya 22 leo baada ya jana
kukwama katika azma yake ya kutaka Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kufanya
marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha uliomnyima dhamana.
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Moshi ndiye
aliyetupilia mbali ombi la Lema, hivyo kumfanya arejee mahabusu huku
mawakili wake wakihaha kuhakikisha wanakata rufaa ili kuomba dhamana
hiyo katika ngazi nyingine ya kisheria.
Aidha,
Jaji Moshi ameridhia ombi la Lema kupitia kwa mawakili wake Sheck
Mfinanga na Peter Kibatala la kukata rufaa mahakamani hapo ili kesi hiyo
isikilizwe na hatimaye Lema kupata dhamana baada ya kupitiwa na jaji
atakayepangiwa.
Akitoa
uamuzi huo mahakamani hapo, Jaji Moshi alisema kimsingi hoja ya
mawakili wa Lema ya kutaka mahakama hiyo kuitisha faili na kulipitia
haina msingi wowote kisheria hivyo anaitupilia mbali hoja hiyo na kutoa
rai kwa mawakili hao kukata rufaa Mahakama ya Rufaa ili dhamana ya Lema
isikilizwe.
“Mahakama
hii haiwezi kupitia faili la kesi hii ya Lema ya kupata dhamana hivyo
siwezi kupitia faili hili, bali nashauri mkate rufaa ili iweze
kusikilizwa,” alisema Jaji Moshi.
Awali
Wakili wa Serikali, Paul Kadushi aliwasilisha pingamizi Mahakama Kuu la
kuitaka wasisikilize maombi ya Lema ya kutaka mahakama hiyo iitishe
faili la kesi namba 440/441 kwa madai yapo makosa ya kisheria
yaliyofanywa awali na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa lengo la
kumnyima dhamana mbunge huyo.
Akiwasilisha
hoja zake mbele ya Jaji Moshi katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,
Kadushi akisaidiana na Materu Marandu alisema anawasilisha hoja mbili za
pingamizi za mahakama hiyo kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
Alisema
kimsingi maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo kutaka mahakama
hiyo iitishe faili la kesi namba 440/441 yanakinzana na kifungu cha 43
(2) cha sheria ya Mahakama ya Mahakimu. Katika kesi hiyo, Lema
anashitakiwa kwa kutoa maneno ya kumtusi Rais katika maeneo tofauti.
Kadushi
alisema uamuzi unaopinga kufanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ya
kukubali kutompa dhamana Lema ni uamuzi mdogo na haukuwa na sababu za
kukataa dhamana.
“Mahakama
yako inafungwa mikono na kifungu hiki kufanya mapitio au uamuzi mdogo,
hivyo tunaomba mahakama itupilie mbali maombi hayo,”alisema Kadushi ambaye wakati akiwasilisha hoja zake alikuwa akinukuu mashauri mbalimbali ya kesi zinazofanana na hiyo.
Aidha,
Kadushi alisisitiza kuwa wao wanatambua haki ya kukata rufaa ipo wazi
kwa mleta maombi ila itakuwa jambo geni kama mahakama itawapa nafasi
kusikiliza maombi yao.
Alisema
hoja ya pili ya pingamizi lake, linatokana na mleta maombi kutokidhi
matakwa ya kisheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Katika
sheria ya makosa ya jinai, kifungu cha 359(1) ya mwaka 2002 kuwa mtu
asiporidhika na maamuzi ya mahakama ya chini kama ilivyo katika kesi
hiyo, kamwe hawezi kuwa na mbadala wa mapitio ya rufaa.
Akijibu
hoja hizo Wakili anayemtetea Lema, Peter Kibatala akiwa na jopo la
mawakili wenzake, Adam Jabir, Sheck Mfinanga, John Mallya, Faraji
Mangula na Charles Adiel, alipinga kuwekewa pingamizi hilo na kuomba
mahakama isikilize maombi yao.
Alisema
wao wamefungua maombi hayo kuiomba Mahakama Kuu kuitisha jalada la kesi
ya mahakama ya chini ili kuona uhalali wa kutotekelezwa kwa uamuzi wa
kutoa dhamana, kwani kilichokuwa kinasubiriwa ni masharti ya dhamana.
“Huyu
mshitakiwa alipewa dhamana , ila kabla ya mahakama haijatoa masharti ya
dhamana, upande wa serikali ukasimama kabla mahakama haijaweka masharti
ya dhamana ambayo lazima ifanye hivyo, wakasema wameonesha nia ya
kukata rufaa na mahakama ikakubaliana nao bila kutekeleza amri yao,” alisema Kibatala.
Aliomba
mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi la serikali na kuiomba kuendelea
na kazi iliyokusudia kuifanya ya kupitia maombi yao ili kutoa dhamana
kwa mshtakiwa au iamuru mahakama ya chini kuendelea na uamuzi wake.
Wakili
wa mbunge huyo baada ya maombi yao kugonga mwamba, walikuwa kwenye
hekaheka ya kukamilisha kuandika rufaa ili kumnasua Lema atoke mahabusu.
Baada
ya kutoka nje ya Mahakama Kuu, Wakili Mfinanga alisema wanamalizia
kukamilisha taratibu za wao kukata rufaa Mahakama Kuu na wataomba rufaa
hiyo isikilizwe kwa hati ya dharura ili kumnasua Lema mahabusu.
Sign up here with your email