Jumla ya Miradi 59 Kutoka Mikoa, Wilaya na Taasisi za Umma Unguja na Pemba imependekezwa kuingizwa katika maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 zinazotarajiwa kuanza mapema mwezi Januari mwaka ujao wa 2017.
Miradi hiyo imeanza kujadiliwa katika Kikao cha kwanza cha Halmashauri ya Kitaifa ya Sherehe na Mapambo Zanzibar kilichokutana kupanga muelekeo wa sherehe hizo kilichofanyika katika ukumbi mdogo ya Jumba la Kasri ya Kifalme liliopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kikao hicho cha Halmashauri ya Kitaifa ya sherehe na Mapambo ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema sherehe za Mapinduzi kwa Mwaka ujao hazitakuwa na tofauti na zile zilizopita za mwaka huu.
Balozi Seif waliwaagiza Wakuu wa Taasisi za Umma pamoja na Wakuu wa Mikoa yote kufanya uhakiki wa ziara katika kuangalia miradi inayoweza kuingizwa katika ratiba ya sherehe hizo kwa ajili ya uwekwaji wa mawe ya msingi au kuzinduliwa rasmi.
Wakichangia mada hizo baadhi ya wajumbe wa Kikao hicho walieleza ni vyema masuala ya Bajeti yakaendelea kujadiliwa na Uongozi wa Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Kamati ya Sekriterieti ili kupata nguvu zitakazowezesha kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Kila Kamati.
Wakigusia suala la Gwaride la Maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar Wajumbe hao walieleza kwamba Vikosi vya ulinzi vinawajibika kukamilisha utaratibu mzima wa Gwaride Kuu kulingana na uzito wa Sherehe husika.
Wajumbe wa Kikao hicho cha Halmashauri ya Kitaifa ya Sherehe na Mapambo Zanzibar wanatarajiwa kukutana tena Tarehe 5 Disemba 2016 kupokea mapendekezo ya Wizara ya Fedha itakayojadiliaja na Kamati ya Sekriterieti ya Halmashauri hiyo sambamba na kupokea Miradi mengine mipya itakayowasilishwa na wajumbe wa Sekta husika.
Wajumbe wa Halmashauri ya Kitaifa ya Sherehe na Mapambo Zanzibar wakijadili muelekeo wa sherehe za Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika katika ukumbi mdogo ya Jumba la Kasri ya Kifalme liliopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kikao cha Halmashauri hiyo ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Balozi Seif kushoto akikiongoza Kikao cha Halmashauri ya Kitaifa ya Sherehe na Mapambo Zanzibar kujadili muelekeo wa sherehe za Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wajumbe wa Halmashauri ya Kitaifa ya Sherehe na Mapambo Zanzibar wakiendelea kujadili mada mbali mbali juu ya muelekeo wa sherehe za Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Picha na OMPR – ZNZ.
Sign up here with your email