LWANDAMINA KOCHA MKUU YANGA, PLUIJM MKURUGENZI BENCHI LA UFUNDI - Rhevan Media

LWANDAMINA KOCHA MKUU YANGA, PLUIJM MKURUGENZI BENCHI LA UFUNDI




HATIMAYE uongozi wa klabu ya Yanga umeweka wazi ujio wa kocha mkuu wa timu hiyo George Lwandamina toka Zambia anayekuja kurithi mikoba ya mholanzi Hans Van De Pluijm anayekuwa mkurugenzi wa benchi la Ufundi.

Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha Redio cha EFM, Makamu  mwenyekiti wa Yanga  Clement Sanga amesema kuwa ni kweli wameingia mkataba na George Lwandamina aliyekuwa akiifundisha Zesco United nchini Zambia na rasmi ataanza kuinoa timu hiyo mzunguko wa pili wa ligi kuu.

Sanga mbali na kuweka wazi suala hilo ambalo lilikuwa ni gumzo kwa vyombo vya habari nchini, pia ametoa maelezo ya kina kwa mustakabali wa aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Hans Van Pluijm na kusema kuwa bado wataendelea kuwa nae kama mkurugenzi wa benchi la ufundi  kwani ni mwalimu mzoefu na anaijua vyema Yanga  hivyo ushauri wake na uzoefu utakuwa chachu ya mafanikio katika benchi letu la ufundi na klabu kiujumla.

Hans Van Pluijm ameridhia nafasi hiyo baada ya uongozi wa klabu hiyo kukaa nae chini na kumwomba aendelee kubaki klabuni kwa nafasi hiyo adhimu kwa maendeleo ya klabu hiyo kimbinu na kiufundi na mabadiliko hayo hayana maana kwamba kiwango cha kocha wa awali  kilikuwa kibaya bali uongozi katika hatua ya kuiboresha klabu yake umeamua kuleta changamoto mpya ili kujiweka bora zaidi katika michuano mbalimbali inayoikabili timu hiyo .

Wakati huo huo makamu mwenyekiti amezungumzia hatima ya kocha msaidizi wa klabu hiyo ndugu Juma Mwambusi bado wanamtambua kama kocha msaidizi wa klabu hiyo mpaka hapo itakapotangazwa tofauti. 

"mara nyingi kocha mkuu ndio anaamua au kupendekeza msaidizi wake na sio klabu hivyo bado Mwambusi ni kocha wetu mpaka hapo itakapotangazwa tofauti . Klabu kwa sasa imejikita kwa hao wawili wakubwa wa juu", amesema Sanga.

Hans Van Pluijm sanjari na Juma Mwambusi wameifikisha timu hiyo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ikiwa nyuma ya wahasimu wao wakubwa Simba SC kwa tofauti ya alama 2  Simba  wanaongoza ligi wakiwa na alama 35 na Yanga 33, kwa sasa uongozi wa Yanga unaandaa siku maalumu ya kuwatambulisha George  Lwandamina kama kocha mkuu na Hans Van Pluijm kama mkurugenzi wa ufundi wa klabu kwa wanachama , wapenzi na wadau wa soka nchini.


Previous
Next Post »