ERICK SHIGONGO AAMUA KUFUNGUKA MAHUSIANO YAKE NA CCM , ADAI WANATAKA KUMDHULUMU HAKI YAKE - Rhevan Media

ERICK SHIGONGO AAMUA KUFUNGUKA MAHUSIANO YAKE NA CCM , ADAI WANATAKA KUMDHULUMU HAKI YAKE

Mwandishi nguli hapa nchini, Eric Shigongo amesimulia masaibu anayoyapitia baada ya kuwa amefanya kazi ya Chama cha Mpainduzi (CCM) lakini hajalipwa fedha zake. Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Shigongo ameandika waraka huu;

Nawaomba radhi sana wananchi wa Singida,  sikuweza kuwepo Namfua baada ya waandaaji kuahirisha tamasha, ipo siku tutakutana.

Nimekwishasema mara nyingi kwamba, hata mimi, kama ilivyo binadamu wengine huwa nina siku mbaya na nzuri katika maisha yangu, kwa sababu kwa watu wengi tafsiri ya maisha bora ni kuwa na gari, nyumba, kazi, fedha nk. Ni rahisi kudhani kwamba ninaishi maisha ya furaha kila siku, si kweli, kuna siku natokwa na machozi kama binadamu mwingine, naomba nikushirikishe sasa siku yangu ya Novemba 19, 2016, siku ya Jumamosi iliyopita, ili upate uhalisia wa maisha.

Usingizi ulikata saa tisa na nusu usiku, nikaanza kuyapitia maisha yangu na changamoto ninazokutana nazo, mambo ninayoyafanya lakini pia kufanyiwa na watu. Mawazo yangu haya yananifikisha kwenye uhusiano wangu na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kwa muda mrefu sana nimekuwa kada wake, mara kadhaa nikijitoa mhanga mimi mwenyewe kukitetea na kukipigania nikiamini ndiyo chama pekee kinachoweza kuwaletea Watanzania mabadiliko ya kweli.

Naipenda CCM, nakiamini chama hiki hata kama kuna baadhi ya watendaji ndani yake natofautiana na jinsi wanavyofanya mambo kiasi cha kuathiri hatma ya chama hiki kama taasisi, wapenzi, mashabiki na wanachama wake.

Pamoja na kuwa mfanyabiashara nimewahi kuacha kazi zangu na kuzunguka karibu nusu ya nchi yetu nikipiga kampeni na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, lakini kwa sababu mtu yeyote anayeonesha mapenzi kwa CCM hasa akiwa mfanyabiashara hutafsiriwa anajipendekeza au mwoga, pengine hivyo ndivyo ninavyoitwa, lakini kwangu mimi ambacho hunisukuma kufanya mambo haya ni mapenzi na imani niliyonayo kwa CCM kama taasisi na zilivyo sera zake.

Kama nilivyosema hapo awali, tatizo langu kubwa huwa ni watendaji wa CCM, ambao wakati mwingine hufanya mambo ambayo huathiri  mapenzi yangu kwa taasisi yenyewe, hali hii imewavunja moyo watu wengi sana waliokuwa na mapenzi pamoja na imani kubwa kwa CCM.

Yesu ni mwokozi wangu, daima nitazungumza ukweli, hata kama utanigharimu! Nakumbuka huko nyuma nimewahi kuzungumza ukweli kuhusu CCM kwenye ukurasa huu, baadhi ya viongozi wa juu hawakufurahishwa na nilichokiandika, Katibu Mkuu Kinana nikiongea naye ofisi kwake aliniambia “Eric wewe ni kijana wa hapa, siku nyingine ukiwa na suala la kuzungumza tueleze sisi moja kwa moja, usilipeleke barabarani!”

Nilikubaliana naye na sikuwa tayari kabisa kusema maneno yaliyotokana na mawazo yangu ya usiku gazetini tena, kwani nilimuahidi nisingefanya hivyo, lakini nifanye nini, nisemee wapi? Kama katibu mkuu wangu nampigia simu kila siku hapokei? Namuandikia ujumbe kwa njia ya WhatsApp na unaonekana umesomwa lakini hanijibu, tafsiri yangu ni ya haraka ni kwamba ananidharau ingawa mimi namuheshimu kama baba  na kiongozi wangu, angalau angekuwa anapokea simu hata kunipa tu matumaini, nisingefikia hatua ya kuzungumza hapa.

Kuanzia usingizi ulipokata saa tisa na nusu usiku, nilifikiria mambo mengi sana juu ya namna ambavyo baadhi ya watendaji wa CCM wamekuwa wakinifanyia pamoja na kujitoa kwangu kote kwa chama hicho, moyo unaniuma mno kwani sistahili hata kidogo kufanyiwa mambo ambayo leo natendewa na chama ambacho mimi binafsi naamini nimejitoa kiasi kikubwa mno kukitumikia kwa akili, muda na mwili wangu.

Inahitaji usiwe mtu mwenye hofu au uliyekata tamaa kufungua mdomo na kuzungumza nitakayoyasema leo, ndugu zangu, Watanzania wenzangu, moyoni mwangu pamejaa uchungu mwingi mno, acha niseme labda nitakuwa mwepesi! Sijui kitakachonipata, Mungu anajua, mimi ni msema kweli, nionavyo mimi ni bora kuzungumza ukweli ukapata matatizo kuliko ubaki hai ukiendeleza unafiki, NASHINDWA.

 Mawazo haya juu ya CCM yananitoa machozi  mke wangu akiwa usingizini kando yangu, sitaki kumuamsha, sitaki kumshirikisha kinachoendelea, mimi ni mtoto wa kiume mambo mengine natakiwa kukabiliana nayo mwenyewe, kwa muda mrefu naendelea kuwaza nikiwapitia viongozi mbalimbali wa CCM kuanzia mwenyekiti mstaafu, mwenyekiti aliyeko madarakani, katibu mkuu na mweka hazina.

 “Mama!” saa kumi na mbili na dakika kumi namuamsha mke wangu.

“Bee!”

“Tulikubaliana kwenda hospitali Muhimbili kusalimia mgonjwa.”

“Kweli.”

“Mzima lakini?”

“Naendelea vizuri, wewe?”

“Mimi mzima, nina mafua tu kidogo!” nilimjibu hivyo kwa sababu sikutaka agundue kilichokuwa kimetokea.

Kawaida ya wanawake ni kujiandaa taratibu sana, mpaka tunaondoka kwenda Muhimbili tayari ilikuwa ni saa moja asubuhi, tumechelewa muda wa kuona wagonjwa. Mbele ya Jengo la Mwaisela, alipolazwa mgonjwa ambaye ni mkamwana wa mama mmoja aitwaye Mama Swai, ambaye tulikuwa tukiabudu naye Kanisa la Word Alive kabla hatujahamia Victory Christian Center, tunakutana na mlinzi mkali kama pilipili.

“Muda wa kuona wagonjwa umekwisha.”

“Tusaidie kaka” nambembeleza kwa muda, hatimaye akionekana kunionea huruma, anasema “basi aende mmoja tu, tena mwanamke, maana hii wodi ni ya wanawake.”

“Mama nenda basi wewe!”

Mke wangu anaondoka na kuniacha nimesimama peke yangu nje ya wodi, mawazo yananirejesha tena kwa CCM baada ya kubaki peke yangu, najiuliza ni kitu gani nimekikosea chama hicho mpaka kunitendea mambo wanayonitendea! Roho inaniuma, nasikia huzuni kubwa moyoni mwangu, niko chini kabisa kiroho leo, sina furaha hata kidogo, mawazo ya CCM na mambo wanayonitendea, wakati mimi nilishafanya mema mengi kwao yamenivuruga.

Dakika ishirini baadaye mke wangu anatokeza kutoka wodini, alikuwa amepewa muda mfupi sana, pamoja tunaongozana mpaka kwenye gari, namfungulia mlango, anaketi nami nakaa kwenye usukani na kuanza kuendesha kuelekea ofisini, anawahi kazini kwake kwa sababu leo ana sherehe ya watu waliokodisha hoteli.

Njiani nasikia wimbo wa vijana kutoka Kenya waitwao Sauti Sol, uitwao ‘Kuliko Jana’ nilishawahi kuusikia wimbo huo kabla, lakini leo unaonekana kuwa wimbo mpya kabisa kwangu, maneno yake yananigusa sana moyo, namshikirisha Vene kwenye wimbo huo, anaonekana kama hanielewi au ninachokiongea hakimgusi, bila shaka anawaza sherehe inayofanyika hotelini kwake.

“Hawa vijana wanaimba sana, natamani siku moja niwaalike hapa Dar es Salaam, nifanye tamasha kubwa la vijana kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu, bure! Nifundishe vijana wa taifa hili uzalendo na kupenda nchi yao.” Natamka maneno hayo ingawa moyoni mwangu kuna uchungu mwingi;

Bwana ni mwokozi wangu,

 Tena ni kiongozi wangu,

Ananipenda leo kuliko jana!

Baraka zake hazikwishi si kama binadamu habadiliki,

Ananipenda leo kuliko jana,

Kuliko jana, kuliko jana,

Yesu nipende leo kuliko jana,

 Kuliko jana, kuliko jana,

Yesu nipende leo kuliko jana,

Nakuomba Mungu uwasamehe

Wangalijua jinsi unavyonipenda

Mimi wasingenisema

Na maadui wangu nawaombea

Maisha marefu wazidi kuniona ukinibariki

Ujue binadamu ni watu wa ajabu sana

Walimkana Yesu mara tatu kabla jogoo kuwika…

Safari inaendelea, wimbo uliokuwa ukipigwa redioni umefika mwisho, kwa kutumia simu yangu nilitafuta ‘You tube’ kisha kuuchagua wimbo huo ambao unaendelea kupiga mpaka namfikisha mke wangu ofisini kwake, kila unapokwisha naurudia tena, unanizidishia uchungu moyoni, namshusha mke wangu na kuendesha tena kuelekea ofisini kwangu.

Mawazo ni mengi, kichwa kimevurugika, Mariam, msaidizi wangu anaingia na kunitayarishia chai, nakunywa lakini haipandi. Baadaye anaondoa vyombo na kuniacha peke yangu, muda mfupi baadaye aliingia mzee Mbizo, sijui kama alinielewa kwa hali aliyonikuta nayo, nilikuwa kwenye siku yangu mbaya, niko chini sakafuni nawaza, baada ya salamu tu tofauti na siku nyingine zote ambazo mimi na yeye huongea mambo machache, anaaga na kuondoka.

Nabaki peke yangu nikiendelea kufikiria, naikumbuka siku ya mwisho nilipofika ofisi ndogo ya CCM pale Lumumba, ambako nilikwenda nikitarajia kulipwa fedha zangu ninazodai kwa kazi niliyoifanya (kwa leo sitataja ni kiasi gani) kama nilivyokuwa nimeahidiwa baada ya kuwa nimesubiri mwaka mmoja na miezi sita, hapo katikati nikiwa nimelipwa fedha kidogokidogo sana.

Tofauti na matarajio kwamba siku hiyo ningelipwa fedha zote, nikalipwa kiduchu tena! Nikiwa ndani ya ofisi ya mweka hazina wa chama, mama Zakia Meghji, yeye ni shahidi, kama nasema uongo au ukweli anajua, machozi yalinitoka! Hali yangu kibiashara ni mbaya, fedha nyingi ziko mikononi mwa CCM na nina madeni makubwa ninayodaiwa, baadhi ya wadai wanataka kupiga mnada mali zangu! Chama Cha Mapinduzi kimeniingiza kwenye matatizo makubwa.

Nakumbuka alichokifanya mama huyu ni kunipa  chupa ndogo ya maji ya Kilimanjaro na kuniambia “Kunywa maji mwanangu, upunguze uchungu!” nikayapokea na kuyanywa, niliondoka ofisini hapo nikiahidiwa kwamba ningelipwa muda si mrefu, lakini haikuwa hivyo, siku zinazidi kusonga na hali inazidi kuwa mbaya na hakuna anayeonekana kujali.

Kwenye saa 5: 00  asubuhi hivi, naamua kuachana na mawazo hayo kwani maisha bado yanaendelea  na kuamua  kwenda kuungana na wenzangu kwenye kikao cha asubuhi kujadili maendeleo ya Gazeti la Ijumaa Wikienda ili nifute kilichokuwa kikiendelea kichwani,  nafanikiwa kufanya kikao hicho bila mtu yeyote kugundua kilichokuwa kikiendelea akilini mwangu na baadaye narejea ofisini ambako naendelea kuusikiliza Wimbo wa Sauti Sol huku nikizidi kuhuzunika.

Muda mfupi baadaye anaingia Davina Lema, msimamizi wa kampuni yetu ya Blue Mark Real Estate ambayo inajishughulisha na upangishaji wa nyumba, tunaongea naye kuhusu biashara na namna ya kufanya biashara katika kipindi hiki kigumu, nampenda Davina, alianza kazi hii akiwa hajui chochote lakini sasa amemudu kazi, baada ya mazungumzo hayo ndiyo naanza kumweleza kidogo kuhusu maisha na namna ambavyo mtu unaweza ukatenda wema lakini ukalipwa ubaya.

Sikuweza kuzungumza hadi mwisho, machozi yananitoka mbele ya mfanyakazi wangu, si jambo jema lakini sikuwa na jinsi, siandiki haya ili nionewe huruma la hasha! Nawaeleza muone baadhi ya siku zangu ambavyo huwa zinakuwa, mtu asinione napita barabarani akadhani maisha yangu ni keki kila siku, kuna mateso na maumivu makubwa nyuma yake!

Alichofanya Davina ni kunitafutia tishu za kufutia machozi kisha kuondoka baada ya meneja wetu mkuu, Abdallah Mrisho kuingia na kunikuta katika hali mbaya niliyokuwa nayo, akaketi chini na kuanza kunidadisi ni kwa nini nilikuwa nalia! Kwikwi ilikuwa imenishika sikuweza kuongea, kuna jitu lilikuwa kooni ambalo nahisi ni hasira.

“Braza inaniuma sana, nimejitahidi maishani mwangu kuwa mtu mwema, nikikusanya senti tanotano kwa njia halali mpaka kufika hapa nilipo, mimi ni tofauti sana na wanasiasa ambao wanaweza kutia saini mkataba mmoja tu wa kifisadi wakaingiza bilioni ishirini au watoto wa viongozi wanaoweza kutumia majina ya wazazi wao kujipatia mikataba minono ya kuwatajirisha, kaka unajua mimi nadunduliza kila siku nikijinyima na kuishi maisha ya kawaida ili niwaachie watoto wangu urithi, leo hii nahisi kabisa nataka kunyang’anywa haki yangu niliyoitesekea kwa muda mrefu, inaniuma!

Kwa mwili huu nilikuwa na uwezo wa kushika bunduki na kuingia benki kuchukua fedha au kwenda Brazil kupakia mzigo mkubwa wa heroin au Cocaine na kuleta hapa nyumbani kuja kuharibu watoto wa watu akili, sikutaka kufanya hayo yote kwa sababu sitaki kufanya dhambi au kupata fedha ambazo baadaye nitajilaumu, nimechagua kufanya biashara halali kuanzia gazeti la shilingi mia moja mpaka leo shilingi elfu moja, kwa nini sasa kikundi fulani cha watu kininyime haki yangu? Sitakubali, ni bora nife kuliko kubaki hai wakati haki yangu inataka kuchukuliwa na wanaoona kwamba wana nguvu na hawawezi kufanywa chochote.”

Wakati nayasema maneno hayo yote nilikuwa nikilia kwa uchungu mno, meneja mkuu alijaribu kunituliza lakini alishindwa, roho ilikuwa ikiniuma sana, mimi mtoto wa maskini, niliyetoka chini kimaisha nikapambana mpaka hapa nilipo, unidhulumu kiasi kikubwa cha fedha namna hiyo? (nitakitaja hivi karibuni). Hapana, ni bora kufa au kupigania haki mpaka tone la mwisho, huko ndiko kunaitwa kuwa mwanaume.

Baadaye nilitulia, tukazungumza na braza Mrisho kwa muda mrefu akinisihi nitulie wala nisichukue hatua yeyote, yeye akiamini haikuwa rahisi kudhulumiwa wakati tulikuwa na mikataba! Jambo moja ambalo hakulifahamu ni kwamba dhamana tulizoweka kwa waliotukopesha fedha zingeweza kuuzwa, hata kama baadaye tungelipwa na CCM ingekuwa haina maana kubwa, wazungu wana msemo usemao “Justice delayed is justice denied” yaani haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki ambayo haikutolewa, wakati wa kulipwa na CCM ni sasa ili tuepuke kuuziwa dhamana zetu.

Alipoondoka meneja mkuu ofisini kwangu, aliingia Nyemo Chilongani, mmoja wa vijana wachapakazi ofisini kwangu ambaye husimamia ukurasa wangu wa Facebook, aliongozana na wasichana wawili ambao aliwatambulisha kwangu kama mashabiki wa ukurasa wangu ambao walikuja ofisini kununua vitabu na walitaka niwasainie vitabu vyao na pia tupige picha pamoja.

Wasichana hawa walikuwa ni Zainabu na Dina kutokea Kigamboni, mara moja nilibadilisha muonekano wangu kama vile kilikuwa hakijatokea kitu, tukaanza kuongea mambo mbalimbali kuhusu maisha, nikiwaeleza umuhimu wa kuthamini vipaji maishani, ambavyo kila mmoja wetu anavyo, “Mtu anaweza kufeli darasani kama nilivyokuwa nikifeli mimi, lakini kipaji kikamuinua na kumfanya awe mtu mwenye mafanikio!”

Mwisho wa mazungumzo yetu nilipiga nao picha na kwa kweli walifurahi kukutana nami ambaye ujio wao na mazungumzo tuliyoyafanya ulisaidia sana  kubadilisha akili yangu na kunipa uwezo wa kuketi chini na kuandika haya unayoyasoma leo.

Hivyo ndivyo siku yangu ya Novemba 19, 2016, ilivyoanza, nifuatilie wiki ijayo nipate kukueleza kwa undani kilichotokea mpaka nikajikuta katika haya niliyoyaandika leo.
Previous
Next Post »