YANGA NA HISTORIA YA KUSHANGAZA - Rhevan Media

YANGA NA HISTORIA YA KUSHANGAZA


AGOSTI 6 mwaka huu Klabu ya Yanga iliweka historia ya aina yake baada ya wanachama wa klabu hiyo kuweka maazimio ya kuikodisha timu yao na nembo kwa Mwenyekiti wao Yusuf Manji.
Manji ameomba akodishiwe Yanga kwa miaka 10 apewe timu na nembo lakini mali na majengo mengine yabaki mali ya klabu kama kawaida. Katika kuikodisha Yanga, Manji ameahidi klabu kupata faida ya asilimia 25 na yeye asilimia 75 na kama ikitokea hasara yeye ndio itakula kwake na sio klabu. Azma ya Manji imekuja baada ya mfanyabiashara mwingine Mohamed Dewji ‘Mo’ kutangaza dau la Sh bilioni 20 kununua asilimia 51 ya hisa za Simba.
Hata hivyo, Manji hakuweka wazi anakodi kwa gharama za kiasi gani, ni nani ambaye atafuatilia kujua ameingiza faida kiasi gani kwenye makubaliano hayo. Kitendo cha Manji kuomba kuikodi Yanga kimekuwa kikiandikwa kwa kiasi kikubwa na kujadiliwa katika mitandao ya kijamii kama suala geni, lakini kwa mujibu wa maelezo yake anasema ni jambo ambalo lipo katika Katiba ya Yanga ya mwaka 2006.
Wanachama wa Yanga waliohudhuria katika mkutano mkuu Agosti 6, 2016 Diamond Jubilee hawakumtendea haki Manji, kwa kutomuuliza mambo matatu kuhusu hoja yake. Mosi, alipaswa kuweka wazi anafikiri ni kwa nini apewe asilimia 75 na sio 25? Kwa nini akodishiwe kwa miaka 10 na sio miwili au mitatu, na Utaratibu gani anataka kuutumia kukodi kama ni fedha angetoa kiasi gani? Maswali ambayo hayakuwepo.
Baadhi ya wanachama wa Yanga wanafurahia, lakini baadhi ya wanachama wengine, wadau na mashabiki wapo kwenye mshangao! Lakini ndiyo hivyo tena, inawezekana siku chache zijazo, klabu hiyo ya kwanza kuanzishwa nchini (1935) ikaweka historia ya kuwa klabu ya kwanza barani Afrika ‘kukodishwa.’ Uamuzi wa kuikodisha klabu hiyo kwa miaka 10 kwa tajiri na Mwenyekiti wa sasa wa klabu, Manji umefikiwa katika mkutano wa dharura Agosti 6 mwaka huu.
Si kwenda kwenye mfumo wa Kampuni na wanachama wanunue hisa kama ambavyo zoezi hilo lililoanzishwa mwaka 2000 ndani ya klabu hiyo baada ya kuisajili kuwa Kampuni huku wana hisa wakiwa ni Francis Kifukwe, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Yanga na wanachama wengine wa klabu hiyo Ibrahim Didi na Lwimbo. Inashangaza lakini upande wangu ‘nimesikitika zaidi’ kwa maana wamedhihirisha ni kwa kiasi gani wanachama wa klabu hiyo wasivyo na hoja.
Ni waoga! Si wadadisi na pengine wana hofu ya ‘maisha bila Manji’. Hivi tujiulize, Manji toka ameingia Yanga mwaka 2006 akiwa mfadhili wa klabu hiyo na baadaye kuingia kwa miaka minne akiwa kama Mwenyekiti wa klabu hiyo mpaka leo haina hata uwanja wake wa kufanyia mazoezi, lakini wanachama hilo hawalioni wao wanashangilia tu kukodiwa kwa miaka 10 na baada ya miaka hiyo ndio waanze kununua hisa, kweli?
Yanga, leo inashuka dimbani kumenyana na Mo Bejaia inafanya mazoezi kwenye uwanja wa kukodi Gymkhana na baada ya mchezo huo sijui itakwenda kukodi Uwanja wa Loyola au Karume kwa ajili ya ligi. Yanga haina uwanja wake wa mazoezi na Manji hadi leo hajawapatia jibu la kueleweka wanachama wa timu hiyo kwa nini anashindwa kuifanyia hilo dogo klabu ambalo lilikuwa miongoni mwa ahadi zake Yanga mpaka leo akodiwe miaka 10.
Manji anafanya mambo makubwa sana ya gharama kubwa Yanga kuliko kuijengea uwanja klabu. Najiuliza kwa nini? Anaingia gharama kubwa kulipia viwanja vya kukodi kila siku lakini angeweza kutumia kiasi cha Sh milioni 30 tu kuifanya Yanga iwe na uwanja wake wa mazoezi.
Yanga ingeweza kununua eneo kubwa nje ya mji na kuotesha nyasi, wakapata uwanja mzuri wa mazoezi lakini suala hilo alipohojiwa na mmoja wa wanachama wakati akinadi sera zake za kukodisha timu alikosa cha kujibu, miaka 10 anairudisha Yanga mikononi mwa wanachama bila uwanja, majengo ambayo ameyaacha kwa klabu maana yake hayamhusu.
Kwa nini Manji kama anataka maendeleo ndani ya klabu hiyo asifufue mchakato wa Kampuni ambao ulishaanza miaka ya nyuma na yeye akaingia kama mmoja wa wana hisa kwa hisa zake za asilimia 40, asilimia 60 zikabaki kwa wanachama au kwenye klabu zikaorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wengine. Kukuza mtaji wa Kampuni, kuweka wazi uendeshaji wa kampuni kwani wanachama wote watakuwa wanajua kila kinachoendelea kwenye kampuni na klabu kwa kuwa soko la hisa linafanya kazi kwa uwazi.
Wadau washangaa
“Kukodi Yanga hili ni suala gumu sana kuliko hata la Simba na linahitaji elimu kubwa zaidi bora la Simba ni suala ambalo watu tunaelewa kuliko la Yanga, ila hili la Manji sijawahi kuona kwa sababu Manji anataka kuchukua timu ya wakubwa na nembo ya Yanga ila mashabiki wanashangilia na hawajiulizi timu yao ya vijana itakuwaje,” anasema mdau wa michezo Edo Kumwembe.
Dk Hamis Kigwangalla: “ Yanga wamekopesha bure, siwaungi mkono, wanampa mtu bure, Simba wananunua hisa wanafanya vizuri, Manji ndio yeye ana sauti kila kitu anaamua yeye, amewashika masikio wana Yanga anafanya kama mali yake hakuna wa kumkosoa wala kumpinga.
Tundu Lissu: “ Sijawahi kuona duniani kote klabu ya michezo ikakodishwa kama lori la kupeleka msiba kijijini”.
Paul Makonda: “Unataka kujua kwa nini Tanzania ni masikini pamoja na utajiri mkubwa iliyonayo? Msome mkataba watakaoingia Yanga.
Zitto Kabwe: “Wanachama wa Yanga wamekubali kumkodisha klabu hiyo Mwenyekiti wao, Yusuf Manji kwa miaka 10 kuanzia leo. Katia utani “Kandambili bana. Sijui akili zao wanaziazimaga? Sasa hizi ni akili au matope? Mnamkodishia mtu timu? Kabisa? Kwa bei gani?”
Hata hivyo mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, Kifukwe anasema wao sio wajinga wakubali kumkodisha Manji bila kujadili mambo muhimu hivyo suala hilo lipo kwenye meza yao na watalifanyia kazi.
Previous
Next Post »