AMOS Makala Mkuu wa Mkoa wa Mbeya amesema mvutano kati ya Serikali na wakulima uliosababisha wakulima hao kutishia kuandamana kupinga kukamatwa kwa magunia yao yanayozidi uzito unakaribia kupatiwa ufumbuzi, anaandika Charles William.
Zoezi la kukamata magunia yanayozidi uzito wa 100 kilogramu limeanza kutekelezwa kwa kasi mkoani Mbeya kufuatia agizo lililotolewa na Majaliwa Kassim Waziri Mkuu wa Tanzania hali iliyoibua malalamiko mengi kutoka kwa wakulima na kutishia maandamano.“Nathibitisha kuanza kukamatwa kwa magunia ya wakulima hao eneo la Uyole na kurudishwa Rungwe ili yakafungwe katika uzito stahiki na wanaokamata mizigo hiyo ni wakala wa vipimo lakini wao hawana Jeshi la Polisi hivyo askari wetu wanafanya kazi,” amesema Makala na kusisitiza;
“Wanaweka ‘lumbesa’ na sisi tunasimamia sheria na agizo la Waziri Mkuu alilolitoa hivi karibuni, lakini kwa kuwa hili suala limezua taharuki tumejipanga kupeleka mizani ya kupimia uzito katika maeneo yao wanayofungia mizigo ili tusiwasumbue kwa kuwakamata barabarani na kuwarudisha wakapunguze uzito wa mizigo.”
Makala amekiri kuwa amri hiyo ya Waziri Mkuu imezua sintofahamu kwa wakulima hao baada ya kuanza kutekelezwa hata hivyo amesema tayari ametuma maofisa wawili kutoka ofisi yake ili wakazungumze na wakulima hao na kuwaelewesha dhamira ya serikali.
“Naamini wakielimishwa wataelewa, wakiambiwa kuwa zoezi hili ni kwa mujibu wa sheria na nia ni kuwasaidia wao kama wauzaji wataelewa tu na kwa kuwa tutaweka vituo vya kupima uzito wa mizigo yao huko huko walipo watatuelewa tu,” amesema.
Wakulima hao walikuwa wakilalamikia kitendo cha serikali kukamata magunia yao yanasafirishwa kwenda sokoni Dar es Salaam na kuwatoza faini ya Sh. 10,000/= kws kila gunia lililozidi uzito wa 100 Kg. pamoja na kuwaamuru warudi shambani na mizigo yao ili wakaifunge upya.
Lakini pia walikuwa wakilalamikia Serikali kuzuia magunia hayo ya wakulima kutoka Mkoa wa Mbeya lakini kuruhusu magunia kutoka mikoa ya mingine ukiwemo Kilimanjaro kuendelea kufungwa kwa mtindo wa ‘lumbesa’ jambo linalowakosesha soko wakulima wa Mbeya.
Akitoa maoni yake kuhusu wakulima wa mikoa mingine kuruhusiwa kuzidisha 100 Kg. huku wale wa Mbeya wakikamatwa na kutozwa faini, Makala amesema anaamini wakuu wa mikoa mingine watatii na kutekeleza agizo hilo la Waziri mkuu Majaliwa Kassim.
“Waziri Mkuu alikuwa hapa Mbeya na akatoa agizo linalotakiwa kutekelezwa na wakuu wote wa Mikoa, agizo la Waziri Mkuu ni kwa wote hata angelitolea Lindi au Rukwa naamini wenzangu watalitii na kulitekeleza pia,” amesema.
Sign up here with your email