MTUHUMIWA WA 'KUIDUKUA' NEC AFARIKI. - Rhevan Media

MTUHUMIWA WA 'KUIDUKUA' NEC AFARIKI.

Udukuzi wa mitandao
Udukuzi wa mitandao

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imepokea Hati ya kifo ya mshitakiwa wa saba katika kesi inayowakabili watu wanaodaiwa kuiba kupitia teknolojia ya mtandao matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka jana kwa lengo la kuyasambaza kabla ya kuthibitishwa na tume ya Uchaguzi (NEC), anaandika Faki Sosi.
Jose Mini (51) raia wa Ufaransa ndiye aliyefariki ambapo yeye na wenzake Mashinda Mtei (49) mkazi wa Tengeru Arusha, Julius Mwita (30) mkazi wa Magomeni Dar es Salaam, Frederick Fussi (25) pamoja na wengineo watatu ni miongoni mwa washitakiwa wa kesi hiyo waliokamatwa tarehe 26 Oktoba 2015.
Respesious  Mwijage Hakimu Mkazi katika Mahakama ya Kisutu amesema kuwa pamoja na kuletwa kwa hati ya kifo lakini mahakama hiyo itafanya uchunguzi na kujiridhisha juu ya  taarifa za hati hiyo wakati Salim Msemo Wakili wa Serikali ameomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa  kesi hiyo.
Kesi hiyo namba 267 ya mwaka 2015 ina mashtaka matatu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii wakati wakijua hazijathibitishwa.
Shitaka la pili linamkabili Matei na Mini, ambapo wanadaiwa kuwa, Oktoba 26  2015  wakiwa katika hoteli ya King iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam wakiwa na hati za kusafirilia zenye namba A1532119 na  M 27687807 walijiingiza katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya CHADEMA kwa ngazi ya urais katika uchaguzi wa mwaka jana.
Shitaka la tatu linamkabili Matei pekee yake ambaye ni raia wa Kenya mwenye hati ya kusafirilia namba A1532119 ambapo anadaiwa kuwa akiwa ndani ya jiji  la Dar es Salaam amekuwa akijihusisha na biashara katika Saccos ya Wanama bila kibali jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Previous
Next Post »