Peter Msigwa Akibebwa na Wananchi katika moja ya mikutano |
Wakati Jeshi la Polisi likitoa masharti hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema vyama vya upinzani vitaendelea kuendesha mikutano ya hadhara licha ya kufungua kesi Mahakama Kuu ya kupinga zuio la shughuli hizo, huku akisema amri ya kuzuia wanasiasa kufanya mikutano nje ya maeneo yao imetolewa bila ya kusoma sheria.
Mkoani Iringa, Jeshi la Polisi lilitoa masharti hayo baada ya Msigwa, ambaye anaongoza Jimbo la Iringa Mjini kwa kipindi cha pili mfululizo, kutaarifu kuwa atafanya mkutano wa hadhara kuanzia Septemba Mosi, siku ambayo Chadema imepanga kuanza operesheni ya nchi nzima inayoiita “ya kupinga udiktekta Tanzania”.
Katika barua aliyomwandikia Mchungaji Msigwa juzi, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Iringa (OCD), Y. Z Mjengi amerejea barua ya mbunge huyo yenye kumbukumbu namba MB/IR/M/05 ya Agosti Mosi mwaka huu, inayohusu mikutano ya hadhara kuanzia Agosti 3 hadi 22, ikianza saa 8:00 mchana hadi 12:00 jioni.
Kupitia barua hiyo, ambayo Msigwa alithibitisha kuipokea, Jeshi la Polisi limesema limeridhia kwa sababu lengo la mkutano wake ni kuhamasisha maendeleo na kupokea kero za wananchi, kazi ambayo inatakiwa kufanywa na mbunge wa eneo husika.
“Natarajia mkutano wako (Msigwa) utakuwa wa amani na utulivu bila kumkashifu mtu wa chama kingine,” anasema Mjengi katika barua hiyo.
“Mikutano yote hiyo kibali kimetolewa kwako kama mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini. Sitarajii mtu mwingine kutoka nje ya Mkoa wa Iringa kuja kukusemea kuhusu maendeleo ya jimbo lako au kuja kupokea kero za wananchi wako na kuzijibia wakati hiyo ni kazi ya mwenye himaya ambaye ni wewe.
“Kashfa, kejeli, matusi na maneno ya uchochezi kwa viongozi wa Serikali vitahesabiwa ni uvunjifu wa amani na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yako na zitapelekea kuzuiliwa kufanya mikutano yako inayoendelea.”
Barua hiyo inaishia kwa maneno yaliyoandikwa kwa herufi kubwa. “Kumbuka: Amani ya Tanzania italindwa na kila Mtanzania kwa hiyo ni jukumu lako wewe Mhe. Mbunge kutekeleza jukumu la ulinzi wa amani. Kwa pamoja tutaweza,” inasema barua hiyo.
Alipoulizwa kuhusu masharti hayo, Mchungaji Msigwa alisema hayo ni ya kwanza lakini hakutaka kuzungumza zaidi kwa maelezo kuwa alikuwa kwenye kikao.
Sign up here with your email