MKATABA WA SUNDERLAND WAITESA TANZANIA - Rhevan Media

MKATABA WA SUNDERLAND WAITESA TANZANIA


maghembenew
MKATABA kati ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Kampuni ya ‘Sunderland Association Football Club’ ya nchini Uingereza ulioidhinishwa mwaka 2013/14 sasa unaitesa bodi hiyo ambayo inadaiwa Sh bilioni 3.7.
Deni hilo limetokana na matangazo ambayo kampuni hiyo iliyatangaza kupitia michezo yake.
Akizindua bodi mpya ya wakurugenzi wa TTB Dar es Salaam jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema mkataba huo ni wa ovyo na sasa unaligharimu taifa.
“Tunadaiwa kwa kuingia mikataba ya ovyo, mkurugenzi aliyekuwepo wakati ule alikataa kuupitisha matokeo yake akafukuzwa kazi, sijui wengine ilikuwaje wakaupitisha na tunapolipa hili deni nadhani kuna mtu hapa nchini anafaidika nalo.
“Sasa kazi ya mwenyekiti wa sasa wa bodi (Jaji Mstaafu Thomas Mihayo) ni kututoa hapa tulipo na kuhakikisha kuwa haturudi tena huko, naiomba bodi hii isije ikakubali kuingia katika mtego kama ule, tumepelekwa mahakamani… tumeshikwa pabaya na lazima tuwalipe sunderland fedha zao,” alisema.
Waziri Maghembe aliitaka bodi hiyo kuhakikisha inatelekeza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vyote vya utalii vilivyoko nchini ili kuongeza idadi ya watalii.
“Andikeni makala pelekeni kwenye mashirika ya ndege watu watazisoma, msikae ofisini nendeni kule viliko, sekta hii ni kubwa mno kwa sasa inachangia asilimia 17 kwenye pato la Taifa tunahitaji ifike asilimia 30 ifikapo 2018,” alisema Profesa Magembe huku akisisitiza litafutwe soko la utalii nchini Urusi na kuimarisha lile la Marekani.
“Nendeni Urusi kutafuta soko si kufanya ‘shopping’ warusi wale wana fedha nyingi na sisi tunahitaji fedha. Najua kuna wakurugenzi watatu wa kitengo cha ugavi, utafiti na sheria wameacha kazi kutokana na kwamba mnaidai serikali, tunajua tutashughulikia.
“Lakini naomba mfanye kazi, tuna vivutio vingi ambavyo hatujavitangaza vema matokeo yake Kenya wanatangaza vingine vipo kwao, tusikubali, lazima muongeze idadi ya watalii kutoka milioni moja iliyoko sasa hadi milioni tatu, nitawapima kwa kazi mkishindwa nitawaondoa wote,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jaji Mstaafu Mihayo alimuomba Waziri Maghembe kuisaidia bodi hiyo kwa kulipa madeni ya wafanyakazi yanayotokana na marupurupu yaliyofikia Sh milioni 300
Previous
Next Post »