SERIKALI kupitia Ofisi ya Mwendesha Mashitaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imetakiwa kufanya utafiti wa kina katika mashauri inayoyafungua mahakamani.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Arusha
jana na Wakili wa Kujitegemea, Charles Abraham, aliyekuwa
akiwawakilisha watuhumiwa 29 katika kesi iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi
ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) na madiwani 28
wa chama hicho wakituhumiwa kuvunja uzio wa thamani ya Sh milioni saba.
Akizungumza
nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya Hakimu
Mkazi, Desder Kamugisha kuifuta kesi hiyo, Wakili Abraham alisema uamuzi
huo ulitolewa baada ya Serikali kukosa ushahidi.
“Ni
rai yangu kwa Serikali kwamba iwe inafanya utafiti katika mashauri
inayoletewa kabla haijapeleka kesi mahakamani. Hii itasaidia kuondoa
gharama zisizo za lazima na usumbufu kwa watu na jamii wakiwamo
viongozi,” alisema Wakili Abraham.
Awali,
mahakamani hapo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Blandina Msawa,
uliwasilisha ombi la kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo, hivyo
ulimuomba hakimu huyo kuiondoa hoja ambayo ilikubaliwa na upande wa
utetezi.
Akitoa
uamuzi wa kuifuta kesi hiyo, Hakimu Kamugisha alisema kwa vile upande
wa mashitaka umeamua kuiondoa kesi hiyo, mahakama haitakuwa na
kipingamizi.
Mbunge Nassari akizungumzia kufutwa kwa kesi hiyo, alisema ilifunguliwa kisiasa badala ya kuangalia maslahi ya mali za Serikali.
Naye
Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Yona Nnko ambaye mwaka jana alihamia
Chadema, alimpongeza Nassari na madiwani kwa kufanikiwa kupigania haki
ya wananchi wa Arumeru Mashariki.
Nassari na madiwani hao walifunguliwa kesi hiyo na Jamhuri wakidaiwa kuharibu mali ya Itandumi Makere katika eneo la Usa River.
Sign up here with your email