MARA: Jeshi la Polisi Kituo cha
Nyamongo, Kanda Maalum Tarime/ Rorya mkoani Mara, linamshikilia
Wang’enyi Juma, 24, (pichani)mkazi wa Wilaya ya Serengeti, Mara
akituhumiwa kumpa mimba mwanafunzi wa Shule ya Msingi Igogo jijini
Mwanza (jina limehifadhiwa), mwenye umri wa miaka 16.
Taarifa zilizothibitishwa na polisi
kanda maalum chini ya kamanda wake, ACP Andrew Satta zinasema kuwa
mtuhumiwa huyo alikamatwa hivi karibuni kisha kufunguliwa jalada la
mashtaka namba NYM/ RB/1491/2016- Kumtia mimba mwanafunzi.
Taarifa zilizotolewa na afisa mmoja wa
polisi aliyekataa kutaja jina lake kwa sababu si msemaji wa jeshi hilo,
zinaeleza kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa, alihojiwa na polisi
kituoni hapo na wakati wowote atapandishwa kizimbani.
“Mtuhumiwa huyo tulimkamata na
tunatarajia kumpandisha mahakamani muda wowote kwa makosa ya kumpa
mimba mwanafunzi …(anamtaja jina),” alisema afisa huyo wa polisi.
Mwanafunzi aliyepewa mimba anasoma
darasa la tano, alianza utoro na baadaye akaacha kabisa shule baada ya
kudaiwa kurubuniwa na kijana huyo, wakawa wanaishi kama mume na mke.
Kaka wa mwanafunzi huyo aliyefahamika
kwa jina moja la Mwita, alikuwa na haya ya kusema: “Huyu kijana
alimtorosha mdogo wetu na kumfanya mke na kwamba hadi sasa hivi
imebainika kwa mujibu wa vipimo vya hospitali, amempa ujauzito, ni
lazima sheria ichukue mkondo wake.”
Mwandishi wetu aliona taarifa ya daktari iliyothibitisha kwamba mwanafunzi huyo ana ujauzito.
Sign up here with your email