WAZIRI Mkuu wa zamani Edward Lowassa, amekutana na kufanya mazungumzo Raila Odinga ambaye ni rafiki mkubwa wa Rais John Magufuli.
Picha mbalimbali zilizotumwa jana na Msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo, zilimwonyesha Lowassa akiwa na Odinga kwenye hoteli moja ya jijini Dar es Salaam.
Lowassa na Odinga walionekana kwenye picha hizo wakiwa wenye furaha kwenye mazungumzo yao na walionekana wakati mwingine wakiwa wamekumbatiana.Msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo alikiri wawili hao kukutana kwenye harusi ya ndugu yake Raila Odinga kwenye hoteli moja jijini Dar es Salaam.
Liongo alisema wawili hao licha ya kwamba walikutana kwenye sherehe lakini walikutana faragha na kuzungumza mawili matatu kuhusu harakati zao za kisiasa. “Wamekutana kwenye harusi hapa Dar es Salaam lakini wamezungumzia harakati zao za kisiasa, Odinga amemweleza mwenzake kuhusu namna walivyoshinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Kenya ijiuzulu na Lowassa pia alimweleza hali ya kisiasa hapa nchini harakati za kisiasa zinazoendelea kwa sasa,” alisema Liongo.
Odinga anatajwa kama mmoja wa marafiki wa karibu sana wa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli tangu akiwa Waziri kwenye serikali ya awamu ya nne.
Sign up here with your email