Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Mang’onyi wakati wa kutatua mgogoro kati ya wananchi na muwekezaji Shanta Gold Mine.
Wananchi wakielemishwa na Mkuu wa wilaya juu ya siasa
zinazokwamisha maendeleo yao huku wanasiasa wenyewe wakishindwa kufanya
uwakilishi katika maeneo yao badala yake wamekuwa wawakilishi wa kitaifa
Msingi wa kikao ni kusikilizana Mkuu wa Wilaya ya
ikungi Miraji jumanne Mtaturu, Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya, Uongozi wa
Shanta Gold Mine na wananchi Kijijini Mang’onyi wakiwa kwenye mkutano wa
kutatua mgogoro wao
Na Mathias Canal, Singida
Mgogoro uliodumu katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi kati ya wananchi wa
Kijiji cha Mang'oni na Muwekezaji Shanta Gold Mine umechukua sura mpya ya
maelewano baada ya wananchi kupatiwa elimu kuhusu umuhimu wa uwekezekezaji na
fursa watakazozipata ikiwa ni pamoja na ajira kwa wananchi wenyewe na maendeleo
ya Vijiji, Kata, Tarafa, Wilaya, Mkoa na Taifa.
Akiwa katika kijiji cha Mang'onyi, Kata ya Mang'onyi Mkuu wa Wilaya ya
Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu
amezungumza na wananchi hao kujua kadhia iliyopelekea kutoelewana kwa kipindi
chote hicho jambo ambalo limerudisha nyuma maendeleo tarajiwa kwa pande zote
mbili.
Mgogoro huo umemalizika kwa Mkuu huyo kuamua kuwa wananchi walipwe fidia
haraka iwezekenavyo ili kupisha uanzishwaji wa Mgodi huo ambapo tayari
takribani wananchi 67 watalipwa katika awamu ya kwanza huku wengi zaidi 130
kulipwa katika awamu ya pili.
Dc Mtaturu amefanya mkutano wake
wa hadhara wa mwanzo tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi ambapo
amewaagiza wawekezaji hao kukutana na kuwa na kikao cha pamoja kati yao na
wananchi waliofanyiwa tathmini kwa ajili ya makubaliano ya namna bora ya malipo
yao ikiwa ni pamoja na kuwashauri kila mmoja kufungua Account Bank ili iwe
rahisi na salama katika uhifadhi wa fedha zao.
Baadhi ya Wananchi katika kijiji hicho cha Mang'oni hivi karibuni walizuia
njia kwa kuweka magogo na mawe barabarani kama ishara ya kuwazuia wawekezaji
hao kupita katika eneo lao kwa madai ya kutolipwa fidia kwa wakati na mwekezaji
kuweka alama za mipaka ya eneo lake pasina wananchi kushirikishwa.
Hata hivyo Dc Mtaturu alisema
kuwa huenda wananchi walikuwa na hoja ya msingi lakini kutolipwa fidia
hakumfanyi mtu kupata uhalali wa kuharibu mali za muwekezaji kwani kufanya
hivyo ni sehemu mojawapo inayochelewesha ulipaji wa fidia.
Mtaturu ameonyesha kukerwa na viongozi wanaowapotosha wananchi hao ilihali
wakiwa wamejificha ama wanaishi mbali na kijijini hapo na kusema kuwa hiyo ni
nidhamu ya woga kwani muwakilishi mzuri wa wananchi ni yule anayetanguliza
maslahi ya wananchi mbele kuliko masalahi ya kisiasa, Chama ama maslahi yake
binafsi.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa kiongozi mzuri daima ni yule anayetatua
changamoto za wananchi sio kuzipinga kwani siasa safi na nzuri ni ile inayoleta
maendeleo sio kupinga maendeleo.
Amewataka wawekezaji hao kuwa na mahusiano mazuri na wananchi kwani
unapokuwa na mradi wako katika Kijiji chochote nchini usipokuwa na mawasiliano
mema na wananchi wa eneo husika ni dhahiri kuwa mradi wako utakuwa hauna
tofauti na mradi mfu.
Hata hivyo pamoja na faida kwa wananchi kulipwa fidia na serikali kupata
pato lake lakini wananchi 60 kutoka Kijijini hapo wataajiriwa katika Mradi huo
kati ya ajira 120 zilizopo ambapo wengine 60 watatoka nje ya eneo hilo ili
kutoa fursa kwa watanzania wote kujipatia ajira.
Sign up here with your email