ASILIMIA 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayotozwa na serikali katika benki na taasisi za kifedha, unaathiri watumiaji wa huduma fedha hususani masikini, anaandika Regina Mkonde.
Hayo yamesemwa leo na Sosthenes Kewe, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Ukuzaji wa Sekta ya Fedha nchini (FSDT) katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa washindi wa shindano la uwekezaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu lililoandaliwa na Soko la Hisa la Dar es Salaam DSE.“Kazi ya kutoza kodi ni ya serikali lakini wakati hayo yanajitokeza tungependa serikali itoe mchanganuo wake na kwa vile mazungumzo juu ya kuitafakari kodi hiyo yanaendelea ni vyema wakaiangalia kutokana na kwamba inaweza ikaathiri watumiaji wa fedha,” amesema.
Kewe ameeleza kuwa, wananchi wengi wanashindwa kujiunga katika mifumo rasmi ya fedha kwa kuhofia vikwazo mbalimbali ikiwemo ukubwa wa gharama.
“Tutapima aina ya vikwazo vinavyosababisha watu wasitumie huduma za fedha na kama gharama ni kikwazo kikuu tutaangalia namna ya kuishauri serikali kurekebisha gharama hizo,” amesema.
“Watanzania wengi hawatumii mifumo rasmi ya fedha kama huduma za kibenki na badala yake hutumia mitandao ya simu, vikoba, na vikundi vya akina mama kuhifadhi fedha zao jambo linalosababisha upotevu wa fedha,”
Amesema kufuatia na hali hiyo kumepelekea baadhi ya watu kupoteza fedha zao kutokana na sababu mbalimbali ambapo kama wangetumia mifumo rasmi wangekuza fedha zao.
“Wengi wanaweka akiba mahala ambapo hapawezeshi akiba zao kukua, huku wengine wakihifadhi fedha zao nyumbani hili jambo si zuri kwa ukuaji na usalama wa fedha, wawekeze kwenye masoko ya hisa ili hapo baadae wapate faida na kukuza mitaji yao ambayo haitakuwa na riba,” amesema.
Francis Maro, Menejea wa Benki ya CRDB ameipongeza DSE kwa kuandaa shindano hilo kwa kuwa linatoa fursa kwa wanafunzi kupata faida ya uwekezaji kwa kuwa sehemu ya wamiliki wa hisa katika makampuni mbalimbali yanayoorodhesha hisa katika soko hilo.
“Huduma za uwekezaji ni muhimu ili kujikwamua kiuchumi na ndiyo sababu ya kuanzishwa kwa shindano hili kwa kuwa walioshiriki wamepata fursa ya kujua namna ya uwekezaji, kuwa wataalamu katika kutathimini sehemu sahihi ya kuwekeza fedha zao pamoja na kuwa wawekezaji wazuri hapo baadae,” amesema.
Amesema, vijana watakapopata elimu ya uwekezaji itasaidia uchumi wa nchi kujengwa na wananchi wenyewe.
Washindi watatu walioshinda leo ni Godfrey Makweka kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha ambaye ameshika nafasi ya kwanza, wakati Benson Humphrey kutoka chuo cha Kilimo cha Sokoine akishika nafasi ya 2 huku Frank Kigodi wa Chuo Kikuu cha Dodoma akishika nafasi ya 3.
Sign up here with your email