WAKATI mashabiki wakitabiri
kiwango cha kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Juma Mahadhi kuwa
kitamuweka benchi Simon Msuva, mwenyewe ameibuka na kudai yeye anamuomba
Mungu asipatwe na majeraha na kitakachofuata wao wenyewe watakubali
mziki wake.
Mahadhi aliyesajiliwa na Yanga hivi
karibuni akitokea Coastal Union, Jumanne ya wiki hii alizua gumzo
kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha katika mchezo dhidi ya TP
Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ikiwa ni mchezo wa Kombe la
Shirikisho Afrika.
Ilikuwa hivi, Msuva alipata ugonjwa wa
malaria muda mfupi kabla ya mchezo huo, ikabidi Kocha Hans van Der
Pluijm amtaje Mahadhi kuwa ataanza katika kikosi cha kwanza, wengi
walipata mshtuko kwa kuwa ilikuwa mechi yake ya kwanza kubwa kuanza
kuichezea Yanga akiwa hana uzoefu hata kidogo.
Kilichotokea baada ya hapo ni kuwa
Mahadhi alionyesha kuwa anaweza ambapo alifanya mambo makubwa licha ya
Yanga kupoteza mchezo huo, hali ambayo ikasababisha wengi wajiulize juu
ya hatima ya Msuva.
Akizungumza na Championi Ijumaa,
Msuva alisema anampongeza Mahadhi kwa kiwango kikubwa alichokionyesha
akicheza mechi yake ya kwanza tangu ajiunge na Yanga kwa kufanikiwa
kuendana na kasi ya timu.
“Mimi kila siku ninamuomba Mungu
nisipatwe na majeraha na siyo kitu kingine, kwa sababu kama nikipata
majeraha ni lazima nikae nje na mchezaji mwingine kuchukua nafasi
yangu,” alisema Msuva na kuongeza:
“Hata simdharau Mahadhi kwani ni
mchezaji mzuri na ninaheshimu uwezo wake ndani ya uwanja, ninafikiri
kila mtu alimuona katika mechi na Mazembe, lakini kwangu hatapata nafasi
ya kucheza labda nipate majeraha makali yatakayonifanya nishindwe
kucheza.
“Ninafurahia changamoto yake ya ndani ya
uwanja inayonifanya nisibweteke zaidi niongeze bidii na kujituma kwenye
mazoezi yangu binafsi na timu.”
Mara baada ya mchezo huo wa Jumanne,
mashabiki na wanachama wa Yanga wengi walionekana kumsifia Mahadhi na
kusema Yanga imepata mchezaji mwenye kiwango kizuri na anayeweza kuwa na
faida kubwa kama ataendelea kucheza kwa kiwango cha juu katika nafasi
ya kiungo mshambuliaji wa pembeni.
Sign up here with your email
