KAIRUKI- WATANZANIA WAUMBUENI WENYE VYETI BANDIA. - Rhevan Media

KAIRUKI- WATANZANIA WAUMBUENI WENYE VYETI BANDIA.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amewaonya watumishi ambao hawaonekani katika vituo vyao vya kazi kuwa watachukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwamo kusimamishiwa mishahara kwa sababu hawafanyi kazi iliyokusudiwa.

Pia amewaomba watanzania wenye taarifa mbalimbali zinazowahusu watumishi wa umma walioajiriwa serikalini kwa kutumia vyeti bandia ama vya majina ya watu wengine kuviarifu vyombo vya ulinzi na usalama, ili viweze kuwachukulia hatua za kisheria na hatimaye kuweza kuwaondoa ndani ya utumishi wa umma.Waziri Kairuki alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wa umma kutoka idara mbalimbali za serikali na taasisi zake juzi mjini Morogoro.

Alisema serikali imekuwa ikifanya mabadiliko ya kiutendaji katika nyanja zote kuweka mazingira wezeshi kwa watumishi wake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kwa lengo la kutoa huduma bora na iliyotukuka kwa wananchi.

Akizungumzia watumishi wenye vyeti feki, alisema ni moja ya mkakati wa serikali ili kuona wote waliingia katika utumishi wa umma wanaondolewa na kubakia na utumishi wa umma wenye sifa na vyeti halali kulingana na taaluma zao walizosomea.

“Vyeti feki sasa ni mwisho kwenye utumishi wa umma …tumeanza kuchukua hatua dhidi ya watumishi wenye vyeti bandia na wapo baadhi wameanza kukimbia, lakini serikali itaendelea kuwatafuta huko waliko ili wafikishwe mahakamani,” alisema.

Kwa upande wa watumishi hewa, aliagiza kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuanza kuchukua hatua za kinidhamu kwa maofisa utumishi waliosababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika maeneo yao ikiwa na kuwafikisha mahakamani kwa kuwa makosa hayo ni ya kijinai


Previous
Next Post »