HOSPITALI YA RUFAA KAGERA YAKABIDHI JENGO JIPYA LA WAZAZI. - Rhevan Media

HOSPITALI YA RUFAA KAGERA YAKABIDHI JENGO JIPYA LA WAZAZI.

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la JhPiego limekabidhi jengo jipya la wadi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera lenye thamani ya Sh mil 136.5, linalotegemewa kusaidia kupunguza msongamano katika wadi ya wazazi, pamoja na vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Ujenzi na upanuzi wa wadi ya wazazi ulifanywa kwa ufadhili wa shirika hilo ambalo ni mshirika wa Chuo Kikuu cha John’s Hopkins cha Marekani.
Akikabidhi msaada huo kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu mwishoni mwa wiki mjini hapa, Mkurugenzi wa shirika hilo, Dk Dunstan Bishanga, alisema lengo ni kuunga mkono jitihada za serikali kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na kuboresha mazingira ya kujifungulia.
Alisema kazi hiyo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jhpiego, Dk Leslie Mancuso ya upanuzi wa jengo hilo ili vitanda vya kulaza akinamama wanapojifungua viweze kuongezwa.
Alitoa ahadi hiyo mwaka jana alipotembelea hospitali hiyo na kujionea wajawazito wakiwa wamelala sakafuni, huku kukiwa na msongamano mkubwa katika wadi ya wazazi.
Alisema hali hiyo ilimsikitisha sana Dk Mancuso na aliahidi ndani ya muda mfupi kukamilisha jengo hilo ambalo ujenzi umefanyika kwa miezi sita.
Jengo lililokabidhiwa lina nafasi ya kuwekwa vitanda 66 tofauti na mwanzo ambapo vitanda vilivyopata nafasi vilikuwa 20 pekee.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Thomas Rutachunzibwa, alimueleza Waziri Ummy kuwa bado katika kitengo cha uzazi kuna changamoto mbalimbali, kwani wadi hiyo moja inatumiwa na wajawazito wenye uchungu wanaosubiri kujifungua, waliojifungua na hakuna wodi ya watoto wachanga.
Rutachunzibwa alisema pia hakuna chumba cha upasuaji kwa ajili ya wajawazito pindi wanapohitaji huduma hiyo kwani hujikuta wakichanganywa na wanaofanyiwa upasuaji mwingine, jambo ambalo ni hatari kwani wao wanahitaji uangalizi wa hali ya juu zaidi.
Ummy alisema kuongeza usawa katika utoaji huduma za afya ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito pamoja na watoto wachanga na wale walio chini ya umri wa miaka mitano ni mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano.
Previous
Next Post »