WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa (Pichani)ameondoka nchini leo (Jumatatu, Juni 27, 2016) kwenda Gaborone, Botswana kuhudhuria mkutano maalum wa wakuu wa nchi na Serikali (extra-ordinary summit) wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kwa niaba ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa atahudhuria kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Double Troika) kitakachofanyika kesho (Jumanne, Juni 28, 2016).
Mkutano huo utafunguliwa na Rais wa Botswana, Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama ambaye pia ni Mwenyekiti wa SADC na utajadili hali ya siasa, ulinzi na usalama nchini Lesotho. Mkutano huu utatanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu ambao unafanyika leo (Jumatatu, 27 Juni, 2016).
Januari 20, mwaka huu, mkutano wa SADC Double Troika uliagiza Serikali ya Lesotho iwe imetangaza matokeo ya Tume iliyoundwa kuchunguza matatizo ya kisiasa nchini humo ifikapo Februari Mosi, mwaka huu. Pia, SADC Double Troika iliitaka nchi hiyo iandae mchakato wa kueleza njia za utekelezaji wa mageuzi kama yalivyopendekezwa kwenye ripoti ya tume hiyo ifikapo Agosti, mwaka huu.
Mkutano huo ulikuwa umepokea taarifa ya Tume ya Usuluhishi ya SADC kwenye mgogoro wa Lesotho iliyoongozwa na Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Dk. Cyril Ramaphosa ambayo iliainisha mambo kadhaa yakiwemo ya kikatiba na kiusalama ndani ya nchi hiyo.
SADC Double Troika ni kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na wakuu wa nchi wanaounda Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation).
SADC Double Troika ni mkutano unaohusisha viongozi wakuu watatu wanaoongoza chombo cha ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama na wengine watatu kutoka kwenye Mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC. Hawa wanawakilisha mwenyekiti aliyepo madarakani, mwenyekiti aliyemaliza muda wake na mwenyekiti ajaye ambaye huwa ni makamu mwenyekiti.
Chini ya muundo wa SADC, kuna mambo makuu mawili; la kwanza likiwa ni utangamano wa kikanda ambao unasimamiwa na mkutano wa wakuu wa nchi (SADC Summit) na la pili ni la siasa, ulinzi na usalama ambalo linasimamiwa na chombo maalum (SADC Organ)
Wajumbe wa mkutano wa SADC Organ ni Msumbiji (Mwenyekiti); Afrika Kusini (Mwenyekiti aliyemaliza muda wake) na Tanzania inayotarajia kuchukua uenyekiti wa chombo hiki ifikapo Agosti, 2016. Botswana, Zimbabwe na Swaziland ndizo zinaunda SADC Summit.
Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Dk. Aziz Mlima na maofisa wengine waandamizi.
Sign up here with your email